Loading...

7/11/2019

Mambo muhimu yatakayokusaidia kufanikisha malengo yakoKila mtu ana mawazo ya kufanikisha kitu fulani. Mawazo hayo baadae huzalisha malengo, na kwa kujiwekea malengo ndio njia ya kufanikiwa katika yale tunayotaka kufanikisha. Kuwa na haja ya kutimiza lako jambo ndio chachu itakayokupelekea wewe kuyaendea  malengo yako bila kusita. Kwakuwa hakuna kitu tunachoweza kufanikisha bila kukifanyia kazi basi ni wazi kuwa hatuna budi kuwajibika ili kutimiza malengo yetu.

Leo napenda kuongelea malengo ya muda mfupi yani malengo ya kukamilisha kwa siku hii ya leo. Siku ya leo ina saa 24 kama zilivyo siku nyingine ila unaweza kufanya siku ya leo kuwa ni bora na yenye tija kuliko zote katika maisha yako.

Maisha ni namna tunavyoishi kila siku, moja wapo ya kitu kinachotuletea maendeleo ni kazi na shughuli mbalimbali za kimaendeleo tunazofanya kila kukicha mpaka jioni. Unaweza kufanya mengi sana uliyoazimia kukamilisha kwa siku ya leo, jinsi utakavyotumia muda wako vizuri kwa kufanya yale unayotaka kutimiza kwa siku ya leo ndivyo utakavyopata mabadiliko makubwa na yenye tija katika kazi zako za siku.

Tumia hizi mbinu mbinu (2) kufanikisha mengi kwa siku ya leo.

1. Panga kazi zako katika hatua ndogo ndogo.
Ili kuepusha mrundikano wa kazi nyingi ambazo nyingine ni kubwa kwako kuweza kufanya kirahisi, ni vyema ukazivunja kazi zako katika hatua ndogo ndogo. Panga kufanya kila kazi katika muda wake. Jiwekee malengo ya kutekeleza kazi zako kidogo kidogo na kuzifanya kwa ufanisi na uhakika.

Ikiwa utaamua kupanga utekelezaji wa kazi zako kwa mpangilio mzuri itakusaidia kurahisisha kumaliza kazi hizo ndani ya muda maalum uliojiwekea. Jua ni kazi gani utafanya kwa dakika 20 na ipi utaimaliza baada ya saa 2 nakadhalika. Kama kila kazi utaifanya kwa wakati wake ipasavyo utaweza kuepuka usumbufu wa mrundikano wa viporo vya kazi ambao sio wa lazima.

2. Weka kipaumbele mambo yako ya msingi unayotaka kukamilisha kwa siku ya leo.
Ni muhimu sana kupanga siku yako mapema kabisa na kwa kuzingatia uhalisia wa kazi au shughuli zenyewe. Pima uzito wa kazi  zote unazotegemea kufanya kwa siku ya leo iwe nyepesi au nzito andika chini kwenye karatasi na jipange namna ya kutekeleza kazi zako, panga kwa makini kazi zako kwa kujua zipi zitachukua muda mfupi kukamilisha na zipi zitachukua muda mrefu.

Katika kuandika malengo yako ya siku ya leo, ni vizuri ukajiuliza maswali haya:
Je ni muda gani unaamka asubuhi?
Je unaweza kufanya nini kwanza kwa muda mfupi baada ya kuamka?
Je huwa unatumia dakika chache kutafakari ni mambo gani muhimu unataka kufanikisha kwa siku?
Je huwa unatumia dakika 10 – 30 kila siku asubuhi kufanya mazoezi ya viungo ili kunyoosha na kuweka mwili wako sawa?

Baada ya kujiuliza maswali yatakayokujenga kiakili na kukusaidia kila siku kusogea karibu na mafanikio ya ndoto zako za maisha ni muhimu kutilia mkazo yale uliyoazimia kuyafanya kwa siku ya leo haijalishi kuwa ni madogo au makubwa, ni vyema ukawa mtendaji na sio mtu wa kuwaza sana bila kutenda. Usidharau udogo wa kazi, ulichoorodhesha kufanya kwa siku ya leo kinamaana kwako kwakuwa ulitafakari na kuandika chini mwenyewe nini unataka kufanya kwa siku ya leo.

Siku ya leo inatakiwa kuwa ni yenye tija na mafanikio makubwa kwako, fanya kazi zako zote za siku ya leo kwa furaha na kwa uhodari. Siku iliokwenda vizuri kwako itahesabika kwa kuzaa matunda kutokana na jitihada zako ulizoziweka katika kufanikisha yako malengo. Ifanye akili yako iamini kile unachotaka kufanya kwa siku ya leo ni sahihi na kinawezekana, Kwa kufanya hivyo utaongeza nguvu ya kufanya mambo yako kwa ufanisi na kwa nia thabiti.
Loading...