NEC yatangaza tarehe ya uchaguzi jimboni kwa Tundu Lissu


Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) imetangaza kuwa tarehe 31 Julai, 2019 ni siku ya kufanyika uchaguzi mdogo Jimbo la Singida Mashariki lililokuwa likishikiliwa na Tundu Lissu baada ya Spika Job Ndugai kutangaza kuwa jimbo hilo liko wazi.

Mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi, Mhe. Jaji (Mahakama ya Rufaa) Semistocles Kaijage alisema kuwa alitoa ratiba ya Uchaguzi huu Mdogo wa Ubunge wa Jimbo la Singida Mashariki kutokana na barua ya Spika wa Bunge inayoeleza kuwa aliyekuwa Mbunge wa Jimbo hilo, Tundu Lissu kapoteza sifa ya kuwa Mbunge kutokana na kushindwa kuwasilisha kwa Spika tamko la mali na madeni na kushindwa kuhudhuria mikutano saba (7) mfululizo ya Bunge bila ruhusa ya Spika.

Jaji Kaijage kwa kuzingatia Katiba ya nchi na Sheria ya Taifa ya Uchaguzi alifafanua ratiba ya Uchaguzi Mdogo huu kwa kueleza kuwa, Fomu za Uteuzi wa Wagombea zitatolewa kati ya  tarehe  13 hadi 18 Julai mwaka huu, Uteuzi wa Wagombea utafanyika tarehe  18, Julai mwaka huu na Kampeni za Uchaguzi zitafanyika kuanzia tarehe 19 hadi tarehe 30 Julai 2019 na Siku ya Uchaguzi itakuwa ni tarehe 31  Julai, 2019.

Aidha, Mwenyekiti, Jaji Kaijage alivikumbusha Vyama vya Siasa na wadau wote wa Uchaguzi kuzingatia Sheria, Kanuni, Maadili ya Uchaguzi, Taratibu, Miongozo na Maelekezo yanayotolewa na Tume ya Taifa ya Uchaguzi wakati wa kipindi chote cha Uchaguzi huu mdogo.