https://monetag.com/?ref_id=TTIb Nitamtuma Waziri Jenista Mhagama aje - Waziri Mkuu | Muungwana BLOG

Nitamtuma Waziri Jenista Mhagama aje - Waziri Mkuu


Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa amesema atamtuma Waziri wa Nchi katika Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia Sera, Uratibu, Kazi, Ajira na wenye Ulemavu, Jenista Mhagama aende Makanya, wilayani Same, kwenye mashamba ya mkonge akatatue kero za wafanyakazi.

“Nitamleta Waziri wa Nchi anayesimamia masuala ya kazi, aje afuatilie kero za wafanyakazi hapa Makanya, manake watumishi wameweka malalamiko yao kwenye mabango na mimi nimeona wanaoendesha mitambo hawana gloves, wengine wamevaa kandambili badala ya mabuti, kofia za usalama nimeambiwa ziko 20 tu,” alisema Waziri Mkuu.

Ametoa ahadi hiyo wakati akizungumza na wafanyakazi wa kiwanda cha kuchakata katani kilichopo kwenye shamba la mkonge la Hasani, kata ya Makanya, wilayani Same, Kilimanjaro, mara baada ya kukagua uzalishaji kwenye kiwanda hicho.

Alifikia uamuzi huo baada ya kusoma mabango yaliyokuwa yakitoa ujumbe juu ya hali mbaya kiwandani zikiwemo malipo ya sh. 3,800 kwa siku; mikataba mibovu ya kazi; wafanyakazi kutothaminiwa wanapougua na kutoridhika na mawakala wawili ambao ni UNIQUE na UPANI waliowekwa kusimamia uendeshaji wa shamba hilo. UNIQUE inasimamia wakata mkonge na UPANI inasimamia kazi ya upandaji na upanuzi wa mashamba.

Hata hivyo, Waziri Mkuu alimweleza Meneja wa Mashamba ya METL likiwemo la Hasani, Bw. Ndekiwa Nyari kwamba uamuzi wa kuweka mawakala unawapunguzia wenye kampuni mzigo wa usimamizi kwenye mashamba lakini unaipa hasara kampuni yao.

“Kwa sasa unashughulika na watu watatu au wanne ambao ni mawakala wakati watu wote wanaokuzalishia wako hapa. Ni vema ungeajiri hao watu wanne, ukawasimamia kwa karibu na unaweza kuwapa motisha wakifanya vizuri au kuwafukuza wakiharibu. Lakini kwa sasa hawa mawakala huna mamlaka hayo, sababu ulishaweka mkataba nao,” alisema.

“Ni bora uwe na idara mbili za upandaji na uvunaji, kisha uweke wasimamizi watatu au wanne ambao watawajibika kwako moja kwa moja. Hii system uliyotumia ina walakini hasa kwenye maslahi ya wafanyakazi. Unawalipa fedha lakini haifiki yote kwa wafanyakazi,” alisema na kuamsha shangwe miongoni mwa wafanyakazi hao.