Prof. Kabudi akanusha kuthibitisha 'kifo' cha Azory Gwanda


Waziri wa Mambo ya Nje wa Tanzania, Profesa Palamagamba Kabudi amekanusha kuwa amethibitisha 'kifo' cha mwanahabari Azory Gwanda.

Msemaji Mkuu wa Serikali, Dkt Hassan Abbas amemnukuu Prof. Kabudi kwa kupitia mtandao wake wa kijamii wa Twitter "Nimepokea kwa masikitiko taarifa potofu zinazoendelea kuchapishwa kwenye mitandao ya kijamii ikinukuu kimakosa mahojiano yangu kwenye kipindi cha BBC FOCUS ON AFRICA zikidai kuwa nimethibitisha kwamba mwanahabari Azory Gwanda amefariki dunia."

"Hii sio tafsiri sahihi kuhusu kile nilichokisema. Katika mahojiano hayo nilieleza kuwa tukio lililotokea Kibiti lilikuwa ni la kuhuzunisha na wapo watanzania waliouwawa na wengine kupotea. SIKUTHIBITISHA kuwa Azory Gwanda amefariki."

"Mpaka sasa hakuna uthibitisho kuwa Azory yuko hai au amefariki. Vyombo vya ulinzi na usalama vinaendelea kuchunguza tukio hilo na matukio mengine yaliyotokea katika machafuko ya Kibiti, Pwani yaliyosababisha ama watu kadhaa kupoteza maisha au kupotea."

Katika mahojiano hayo ambayo yalirushwa jana Alhamisi Julai 10, 2019 Profesa Kabudi alisema kwa kingereza kuwa mwandishi huyo "has disappeared and died" ikiwa na maana kuwa 'alitoweka na kufariki'.

"Azory Gwanda ni sehemu ya Watanzania wengine wengi ambao wameuawa katika eneo lile (kibiti)," alisema Kabudi na kusisitiza kuwa yaliyotokea Kibiti na Rufiji ilikuwa ni kipindi cha uchungu zaidi katika historia ya Tanzania.

''Wacha nikwambie unapozungumzia kuhusu kisa hicho, ni mojawapo ya visa ambavyo vimesababisha uchungu mwingi nchini Tanzania,'' alisistiza Prof Kabudi.