Tanesco Babati yamnasa Fundi Feki aliemkatia mteja Umeme

Tanesco wilaya ya Babati mkoani Manyara wamefanikiwa kumkamata kijana mmoja aliejitambilisha kwa jina la John Mauki (29) aliejifanya fundi umeme na vifaa vinavyotumia umeme na  kujipatia shilingi laki moja kutoka kwa mwenye nyumba Eng.Mathew Tillya.

Tillya alisema kwamba Kijana huyo alifika nyumbani kwake mtaa wa Nyunguu mjini Babati na kujitambulisha kuwa yeye ni fundi wa vifaa vinavyotumia umeme,ndipo alipomuonyesha Tv na Redio ambazo zilikuwa mbovu ili azitengeneze lakini matokeo yake mtu huyo anaejiita Fundi alifungua vifaa hivyo bila kufanikiwa kutengeneza na kudai kuwa nyumba hiyo ilikuwa na hitilafu ya umeme.

Ameendelea kusema kuwa kutokana na tatizo hilo mtuhumiwa aliomba apewe kazi ya kurekebisha tatizo hilo,ambapo licha ya kukataliwa aliamua kuchukua vifaa vyake alivyonavyo na kukata waya za mita zinazoingiza umeme kwenye nyumba hiyo.

Amesema baada ya kuona kuwa mtu huyo sio fundi akashirikiana na majirani zake kuweka mtego wa kumkamata kesho yake na kuwaita watu wa Tanesco.

Mtuhumiwa huyo alipoulizwa kwanini ameamua kufanya hivyo,alidai kuwa yeye ni fundi na amekuwa akifanya kazi hizo kwa muda mrefu.

Kwa upande wa Afisa uangalizi wa Tanesco mkoa wa Manyara Ernest Massawe,amesema kuwa sio ruksa kwa fundi yeyote kugusa mita za Tanesco na endapo kuna tatizo taarifa itolewe kwenye ofisi za Tanesco nao watatuma mafundi wao wenye taaluum yaUmeme.

Hata hivyo mtuhumiwa amefikishwa kituo cha polisi Babati akisubiri kufikishwa mahakamani  kwa taratibu nyingine za kisheria.