Waandishi wa Habari waaswa kuzingatia uzalendo na weledi


Waandishi wa Habari nchini wameaswa kuzingatia uzalendo na weledi  katika utekelezaji wa majukumu yao  wakati wote wa kuripoti habari zinazohusu fursa zilizopo katika Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC)  pamoja na mkutano wa wakuu wa nchi wanachama utakaofanyika Jijini Dar es Salaam Agosti 17 na 18, 2019.

Akizungumza mjini Morogoro wakati akifungua awamu ya kwanza ya mafunzo yakuwajengea uwezo  waandishi wa habari ili waweze kuandika na kuripoti habari za Jumiya hiyo, Naibu Waziri wa Habari Utamaduni Sanaa na Michezo, Juliana Shonza amesema  kuwa mkutano wa Wakuu wa nchi wanachama unakuja na fursa nyingi zitakazowanufaisha wananchi wote.

“ Tunawaomba Waandishi wa Habari kutekeleza jukumu la kutangaza habari zinazohusu SADC kwa uzalendo, weledi na kwa ufanisi ili watanzania waweze kushiriki kikamilifu kutokana na umuhimu wa Jumuiya hii na kutumia fursa za kiuchumi na biashara zinazopatikana kupitia wananchi takribani milioni 450 wa nchi zote za SADC”Alisisitiza Shonza.

Akifafanua Mhe Shonza amesema kuwa  kila mwandishi wa habari analo jukumu la kuhakikisha kuwa kila mwananchi anafahamu fursa zilizopo katika Jumuiya hiyo na mamna zinavyoweza kuwanufaisha wananchi wote katika nyanja za kiuchumi na kijamii.

Aliongeza kuwa  waandishi wa habari wa Tanzania kuna umuhimu mkubwa wa kuwa na uelewa wa pamoja wakati wa mkutano huo  kwa kutambua kuwa wao ni daraja kati ya wananchi na Serikali pamoja na Jumuiya zote ambazo Tanzania ni mwanachama ikiwemo SADC.

“Ni matumanini yangu kuwa baada ya mafunzo haya mtawaelimisha wananchi kuhusu umuhimu wa SADC kwa maendeleo ya kiuchumi ya nchi wanachama, fursa za kiuchumi, Namna nchi yetu inavyotekeleza mikakati mbalimbali ya SADC, Fursa za masoko ndani ya SADC kutokana na bidhaa na mazao ya kilimo yanayozalishwa katika nchi wanachama,” Alisisitiza Shonza.

Katika kusisistiza umuhimu wa amani na utulivu, Shonza aliwaasa wanahabari kuwaelimisha wananchi umuhimu wa amani kipindi choche cha mkutano huo wa wakuu wa nchi wanachama na hata baada  ili kuendelea kujenga taswira nzuri ya Tanzania.

Baadhi ya fursa zinazotokana na mkutano wa 39 wa wakuu wa nchi wanachama wa Jumuiya hiyo utakaofanyika mwezi ujao hapa nchini ni pamoja na usafiri na usafirishaji, malazi na utalii kwa wageni hao zaidi ya 1000 wanaotarajiwa kuja hapa nchini kutokana na mkutano huo.

Aidha, Mheshimiwa Shonza aliwataka waandishi wote wa habari hapa nchini kutumia nafasi zao kuwaelimisha wananchi kuhusu umuhimu wa amani iliyopo hapa nchini ambayo ni moja ya kivutio kikubwa kwa wageni kutoka mataifa mbalimbali kuja na kuwekeza hapa nchini.