https://monetag.com/?ref_id=TTIb Walemavu waiomba Tume ya Uchaguzi kuweka Mazingira Rafiki | Muungwana BLOG

Walemavu waiomba Tume ya Uchaguzi kuweka Mazingira Rafiki



Na. Ferdinand Shayo,Arusha.

Walemavu mkoa wa Arusha wameiomba Tume ya uchaguzi  kuweka mazingira rafiki kwa walemavu ili waweze kushiriki katika zoezi la uandikishaji wa daftrari la wapiga kura na kutimiza haki yao ya kikatiba bila kupata vikwazo vinavyotokana na ulemavu wao.

Akizungumza katika kikao cha Tume ya Uchaguzi na wadau wa Uchaguzi wakiwemo wawakilishi wa vyama vya siasa,wawakilishi wa makundi maalumu katika jamii,Katibu wa Shirikisho la vyama vya  Walemavu Wilaya ya Arusha Yunisi Urassa ametoa maombi hayo huku akisisitiza kuwepo kwa mazingira rafiki katika vituo vya kujiandikisha ili viweze kufikika kwa urahisi na watu wote

 Mkurugenzi wa Daftari wa Tehama Tume ya Uchaguzi Martin Mnyenyelwa amesema kuwa serikali imejizatiti na kuweka mazingira rafiki ikiwemo karatasi za nukta nundu kwa ajili ya walemavu wasioona pamoja na kuwapa kipaumbele watu wenye ulemavu kuhudumiwa kwanza kabla ya watu wengine.

Makamu Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi Taifa Mbarouk Salim  amesema kuwa zoezi hilo litaanza hivi karibuni na tayari ziko asasi za kiraia zilizopewa kibali cha kutoa elimu za raia kwa wapiga kura ili waweze kutumia haki yao ya kikatiba.

Wajumbe kutoka katika vyama vya siasa Denis Mwita Katibu wa Ccm wilaya ya Arusha na Innocent Joseph  ambaye ni Katibu  wa Chadema Wilaya ya Arusha wameiomba tume hiyo kuweka vituo karibu na makazi ya wananchi pamoja na kuhakikisha kuwa sheria za Uchaguzi zinazingatiwa.