Apigwa risasi na kufariki kwa kumcheleweshea mteja sandwich yake

Muhudumu mmoja wa mgahawa mjini Paris amepigwa risasi hadi kufa na mteja ambaye amedaiwa kwamba alikuwa amekasirishwa kwa kuwa sandiwich yake haikuandaliwa haraka iwezekanavyo.

Maafisa wa polisi wanasema kwamba uchunguzi umeanzishwa baada ya tukio hilo siku ya Ijumaa jioni mashariki mwa eneo la Le-Grand.

Mshukiwa alitoroka katika eneo hilo na hajapatikana.

Wafanyakazi wa ambalensi walijaribu kuokoa maisha ya muhudumu huyo ambaye alikuwa amepigwa risasi katika bega lake lakini alifariki papo hapo.

Wenzake waliambia maafisa wa polisi kwamba mteja huyo alikuwa na hasira katika duka hilo la Pizza na Sandwich kutokana na muda mrefu ambao sandwich hiyo ilichukua kuandaliwa.

Mauaji hayo yamewashangaza wakaazi na wamiliki wa maduka.

'' Inasikitisha'' , mwanamke mmoja mwenye umri wa miaka 29 aliambia chombo kimoja cha habari nchini Ufaransa .

''Ni mgahawa uliotulia sana na hauna matatizo. Ulifunguliwa miezi kadhaa iliopita''.

Baadhi ya wakaazi, hatahivyo wamesema kwamba kumekuwa na ongezeko la visa vya uhalifu katika eneo hilo mbali na ongezeko la visa vya ulanguzi wa mihadarati pamoja na unywaji pombe barabarani