https://monetag.com/?ref_id=TTIb Dkt.Gwajima: Simamieni kwa weledi utekelezaji wa miradi ya Global Fund | Muungwana BLOG

Dkt.Gwajima: Simamieni kwa weledi utekelezaji wa miradi ya Global Fund



Na Angela Msimbira OR-TAMISEMI

Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa anayeshughulikia afya Dkt. Dorothy Gwajima amewaagiza waratibu wote wa miradi ya Afya chini ya Mfuko wa Dunia wa Kupambana  na Ukimwi, Kifua Kikuu na Malaria kusimamia utekelezaji kwa weledi  ili kuhakikisha walengwa wanapata huduma bora kwa wakati na kuongeza kasi ya kudhibiti magonjwa haya kwa Kinga na Tiba.


Ameyasema hayo leo wakati akifunga kikao kazi  cha kujadili  utekelezaji wa shughuli  za Mfuko wa Dunia  wa Kupambana  na Ukimwi, Kifua Kikuu  na Malaria kilichofanyika katika Ukumbi wa Mikutano wa Chuo cha Mipango , Jijini Dodoma.

Amesema kuwa, Vita dhidi ya magonjwa haya itafanikiwa zaidi iwapo kila mmoja atawajibika katika nafasi yake na kuhakikisha shughuli zilizopangwa zinatekelezwa kwa wakati na ufanisi na taarifa husika zinatolewa kwa wakati na ubora.

Dkt. Gwajima amesema, viongozi wote ngazi ya Halmashauri wahusike na utekelezaji wa miradi hii kwa kuwa, siyo suala la wataalamu wa afya pekee bali sekta zote wakiwemo Wakurugenzi wa Halmashauri, Maafisa Mipango wa Halmashauri na Waweka Hazina wa Halmashuari.


Amesisitiza kuwa, katika safari ya kuelekea kwenye nchi ya viwanda na uchumi wa kati, sekta ya afya ni mdau mkubwa kwa kuwa, kadri wananchi wenye uhitaji wanavyopata huduma bora za afya kwa wakati na kadri wanavyoepuka maradhi ndivyo wanavyoongeza kasi ya safari hiyo hivyo, kila anayeshindwa kuongeza kasi ya utekelezaji wa miradi hiyo anapunguza kasi ya safari hiyo na atachukuliwa hatua.

Dkt. Gwajima amezipongeza halmashauri 85 ambazo zimefanya vizuri kwenye utekelezaji wa mradi huo kwa kasi kubwa na amezitumia salaam halmashauri zingine 100 ambazo zimesuasua  kwenye utekelezaji wa miradi hiyo na kuwataka  kuandaa maelezo ya kutosha kwa nini wasihesabiwe kuwa wanakwamisha safari ya nchi kwenda kwenye viwanda na uchumi wa kati kwa kuchelewesha huduma.

 “Nimesikitishwa na Baadhi ya Halmashauri nchini ambazo zina kasi ndogo ya kutekeleza miradi hii na ninachokiona hapa ni uzembe tu ambao itabidi wahusika wawajibike, kwa nini wengine watekeleze kwa wakati na ufanisi wengine wabaki nyuma” Amehoji Dkt. Gwajima

Wakati huohuo, amewaagiza Waganga Wakuu wa Mikoa na Wilaya na Waratibu wote wa Miradi hiyo kuwa, wakumbuke nafasi walizonazo ni kama ibada kwa kuwa, zinahusisha masuala ya uhai na uponyaji hivyo, wasimamie kikamilifu utekelezaji wake na kuwashirikisha viongozi wote na kufanya kazi kwa ushirikiano ili kuunganisha nguvu katika kukabiliana na changamoto za utekelezaji.

Aidha amewahimiza kuwasilisha taarifa za utekelezaji zikiwemo stakabadhi za kukiri mapokezi ya fedha kwa wakati.