Halmashauri zote ambazo hazijalipa kodi ya pango kubanwa


HALMASHAURI ZISIZOLIPA KODI YA ARDHI KATIKA MAENEO YA BIASHARA KUBANWA

Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula ameagiza Halmashauri zote nchini ambazo hazijalipa kodi ya pango la ardhi katika maeneo yake ya biashara kufikishwa Baraza ya Ardhi ya Nyumba la Wilaya ili kulipa kiasi inachodaiwa.

Dkt Mabula alitoa agizo hilo katika halmashauri ya Wilaya na Mji Nzega mkoani Tabora wakati wa ziara yake ya kuhamasisha ukusanyaji maduhuli ya serikali kupitia kodi ya ardhi pamoja na kukagua masijala ya ardhi.

Alisema, halmashauri zinatakiwa kuonesha mfano wa kulipa kodi ya pango la ardhi kwa kuwa baadhi yake zinakusanya mapato katika maeneo ya kibiashara lakini hazilipi kodi hiyo jambo alilolieleza linaenda kinyume na utaratibu.

Kwa mujibu wa Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi, msamaha kwa taasisi ambazo hazipaswi kulipa kodi ya pango la ardhi una utaratibu wake  na kila halmashauri inapaswa kulipa kodi inayodaiwa katika maeneo ya kibiashara ambapo alifafanua kuwa hata zile taasisi za dini zinazofanya biashara nazo zinapaswa kulipa isipokuwa kwa maeneo yake ya kuabudia.

"Tutafuatilia halmashauri zote ambazo hazilipi kodi ya pango la ardhi katika maeneo yake ya biashara, unawezaje kudai wengine wakati wewe hulipi? Kama hamjaweka utaratibu wa kulipa muweke’’ alisema Dkt Mabula.