Mama auwawa kwa tuhuma za uchawi, Watatu wafikishwa kortini


Watu watatu wamekamatwa na kufikishwa Mahakama ya Wilaya ya Igunga kwa tuhuma za mauaji ya mama wa miaka 55 Wilayani Igunga Mkoani Tabora.

Wakazi wa Kijiji cha Kitangili, waliofikishwa mahakamani mwishoni mwa wiki, ni Sung’hwa Ngassa (54), Willson Sunhwa (30) na Sunhwa Nzumbi (39) wote wakulima.

Mwendesha Mashtaka wa Polisi, Elimajid Kweyamba, mbele ya Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Igunga, Lydia Ilunda, alidai washtakiwa wote kwa pamoja walitenda kosa hilo kinyume na kifungu cha 196 kanuni ya adhabu sura ya 16 mapitio ya 2002.

Alidai Julai 28, mwaka huu saa 6:30 usiku katika Kijiji cha Kitangili, washtakiwa walimuua Veronica Makumbi (55) mkazi wa Kitangili, baada ya kumtuhumu kuwa ni mchawi.

Baada ya kusomewa shtaka hilo, washtakiwa wote kwa pamoja hawakutakiwa kujibu kitu chochote kwa kuwa mahakama hiyo haina mamlaka ya kusikiliza shauri hilo.

Kesi iliahirishwa hadi Agosti 29, itakapotajwa tena na washtakiwa walipelekwa mahabusu.