Matukio ya moto yazidi kuzuka katika msitu wa Amazon

Mamia ya matukio mapya ya moto yamezuka tena leo katika eneo la msitu wa Amazon kaskazini mwa Brazil, wakati jamii ya kimataifa ikiendelea kumuekea shinikizo Rais Jair Bolsonaro kuuzima moto huo ambao ndio mbaya kabisa kuwahi kushuhudiwa katika miaka mingi.

Moto huo wa msitu wa Amazon umetawala mkutano wa kilele wa nchi za G7 unaoanza leo nchini Ufaransa.

Takwimu rasmi zinaonyesha kuwa matukio 78,383 ya kuwaka moto yamerekodiwa nchini Brazil mpaka sasa, ikiwa ni idadi kubwa kabisa kushuhudiwa katika mwaka wowote tangu 2013.

Takwimu hizo mpya zimetolewa siku moja baada ya Rais Bolsonaro kuamuru wanajeshi kwenda kusaidia kukabiliana na moto huku akitupia lawama hali mbaya ya ukame kusababisha janga hilo la asili.

Bolsonaro amesema serikali ilikuwa inajua kabisa kuhusu hali ilivyo na itakabiliana na kile alichokitaja "uhalifu wa kimazingira" sawa na namna ambavyo hukabiliana na uhalifu mwingine wa kawaida.