Mbunge Matiko aomba Hospitali kupandishwa hadhi


Na Timothy Itembe, Mara

Mbunge  wa jimbo la Tarime Mjini, Esther Matiko ameshauri Serikali kuipandisha hadhi hospitali ya wilaya inayomilikiwa na halmashauri ya Mji wa Tarime ili  kukidhi mahitaji ya huduma ya  matibabu kwa wagongwa.

Matiko alitoa ushauri huo jana katika kikao cha Baraza la Madiwani cha kawaida cha kufunga mwaka ambapo alisema kuwa kutokana na hospitali hiyo kulemewa na wagonjwa kuna haja serikali kuipandisha hadhi na kuwa hospitali ya kanda maalumu mkoa wa Afya Tarime na Rorya kama ilivyounda mkoa wa kipolisi Tarime na Rorya.

"Mimi nishauri Baraza lako mwenyekiti kunikubalia ushauri wangu ili kufanyike mchakato wa kuandika andiko kwenda Serikalini juu ya kupandishwa hadhi hospitali yetu kutoka hospitali ya wilaya na kuwa hospitali ya kanda maalumu ya Afya Tarime na Rorya kama ilivyoundwa mkoa wa kipolisi Tarime na Rorya lengo ni letu ni kuwa ikidhi mahitaji ya wagonjwa kwani ilivyo inalemewa na wagonjwa kutoka halmashauri ya Tarime vijijini wengine kutoka Rorya,Serengeti na hata kutoka Nchi jirani ya Kenya kuja kutibiwa huku"alisema Matiko.

Matiko aliongeza kuwa hospitali hiyo inalemewa na wagonjwa ikilinganishwa na ruzuku inayotolewa na serikali kuwa nindogo na inatolewa kwa kata nane za halmashauri ya Tarime mjini lakini wagonjwa wanaokuja kutibiwa hapo ni wengi kuliko.

Naye mwakilishi wa mganga mkuu wa hospitali ya Wilaya inayomikiliwa na halmashauri ya Mji,wa Tarime,Jushwa Makoa ambaye pia ni mtaalamu wa maabara alilikiri hospitali hiyo kulemewa na wagonjwa wengi ambapo wengi wao wanatoka  halmashauri ya Tarime vijijini huku wengine wakitoka wilaya za Serengrti,Rorya na Nchi jirani ya Kenya ambapo wote ni majirani.

Makoa aliongeza kuwa kutokana na ujirani mwema uliopo baina ya halmashauri ya Tarime Mjini na wilaya za Serengeti,Rorya halmashauri ya Tarime Vijijini  na hata Nchi jirani ya Kenya wanalazimika kutoa huduma kwa wagonjwa wao badala ya kuwarudisha kwenda kutibiwa maeneo yao huku wanakotoka ambapo wanalazimika kutoa huduma kwasababu hospitali lengo lake ni kutoa huduma kwa jamii.

Makoa alikiri kuwa wanapokea Ruzuku ya fedha kutoka serikalini ambayo inakuja kwa idadi ya watu wa kata nane zilizopo ndani ya halmashauri ya Tarime Mjini.

Kwa upande wake mwenyekiti wa halmashauri ya Trime Mjini,Khamisi Nyanswi alisema kuwa hospitali hiyo ikipandishwa hadhi watapata fedha ya ruzuku nyingi kutoka serikalini tofauti na fedha inayokuja ya watu wa  kata Nane tu na kuwa hospitali hiyo itakuwa na madawa ya kutosha katika tiba ya Mama na mtoto,huduma kwa wazee pamoja na wamama wajawazito na watoto chini ya umri wa miaka mitano inayotolewa na serikali.