Naibu Waziri Masauni asisitiza utoaji elimu barabarani kupunguza ajali


Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Hamad Masauni amesema kuna kila sababu ya kuendelea kutolewa elimu ya usalama barabarani na matumizi sahihi ya barabara ili kupunguza ajali zinazosababisha ulemavu na vifo kwa watu wasio na hatia.

Pia alisema wizara hiyo ipo kwenye mchakato wa kuangalia upya sheria za usalama barabarani kwa lengo la kuziongezea ukali ili kukabiliana na watumiaji wa vyombo vya moto na hasa waendesha pikipiki ambao wengi wao wamekuwa wakivunja sheria na kusababisha ajali ambazo zinaweza kuepukika.

Masauni aliyasema hayo wakati wa utoaji zawadi kwa wanafunzi na shule za msingi ambazo zimeshinda michoro yenye ujumbe wa usalama barabarani visiwani Zanzibar mwaka huu.

Shule ya Msingi Mkunazini ilipata Sh. milioni 4 kutoka Kampuni ya Mafuta ya Puma Tanzania, baada ya kuibuka mshindi wa kwanza.

Mafunzo ya elimu ya usalama barabarani yanayofadhiliwa na Kampuni ya Mafuta ya Puma Tanzania ndiyo mara ya kwanza kutolewa visiwani humo.

“Kuna umuhimu mkubwa wa jamii yetu ya Watanzania kwa upande wa Bara na Visiwani kuendelea kupatiwa elimu inayohusu usalama barabarani pamoja na matumizi sahihi ya barabara zetu.

“Nitumie nafasi hii kuipongeza Kampuni ya Puma Tanzania kwa uamuzi wake wa kutoa elimu hii ambapo kwa hapa Zanzibar shule tano za msingi zimepata elimu hiyo na tunaamini itasaidia kupunguza ajali ambazo zinaweza kuepukika,” alisema.

Alisema kutolewa elimu ya usalama barabarani kwa wanafunzi kutasaidia kuokoa maisha yao na kuwaepusha na ajali.

"Ajali za barabarani zimeendelea kupungua siku hadi siku, lakini bado kuna changamoto ya baadhi ya watumiaji wa vyombo vya moto na hasa waendesha bodaboda wanavunja sana sheria za barabarani."

“Tumeamua atakeyakamatwa kwa kuvunja sheria za usalama barabarani awekwe mahabusu, kisha apelekwe mahakamani ili sheria ichukue nafasi yake,” alisema.