https://monetag.com/?ref_id=TTIb Ruksa kufanya biashara saa 24 Iringa | Muungwana BLOG

Ruksa kufanya biashara saa 24 Iringa


Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Ally Hapi ametangaza uamuzi utakaoruhusu biashara za burudani mjini Iringa zifanyike kwa saa 24 ili kuchangamsha mji huo ambao ni lango kuu la utalii wa mikoa ya Nyanda za Juu Kusini.

Hivi sasa biashara nyingi zinafanyika kati ya saa 10 jioni na saa tano usiku, hatua ambayo imeleta usumbufu kwa watoa huduma wa kabla na baada ya muda huo.

Uamuzi wa Mkuu wa Mkoa huyo umepokelewa kwa nderemo na vifijo na baadhi ya wafanyabiashara wa vileo ambao pamoja na wateja wao walikuwa wakipata misukosuko ya mara kwa mara kutoka kwa Polisi na mamlaka zingine zinazosimamia utaratibu huo wa muda huo.

Mmoja wa wafanyabiashara hao, Anselim Makingi wa Luxury Bar, alimpongeza Mkuu wa Mkoa akisema uamuzi huo utarudisha mzunguko wa biashara uliopotea, utaboresha makusanyo ya mapato yao na serikali na ni wa uhakika kwa wateja wanaohitaji huduma hiyo kabla ya saa 10 jioni na baada ya saa tano usiku.

Makingi alisema baa za siku hizi zina vitu vingi vinavyorahisisha maisha ya mnywaji kama vile chakula cha asubuhi, mchana na jioni, huduma za fedha kupitia mitandao ya simu, huduma ya kinyozi na kutengeneza nywele na nyinginezo lakini zote hizo zilidolora kwa sababu ya udhibiti wa muda.

Akizungumzia uamuzi huo kwenye kikao cha Halmashauri Kuu ya CCM Mkoa wa Iringa wakati akitoa taarifa ya utekelezaji wa Ilani ya CCM ya kati ya Januari na Desemba mwaka jana, Hapi amesema amepanga kukutana na wafanyabiashara wa maeneo ya burudani hivi karibuni ili awaruhusu wafanye biashara zao kwa saa 24.

"Nataka Iringa ichangamke, watu wafanye biashara muda wote haya mambo ya kukamatakamata watu na wengine walioko kwenye starehe zao kulazimishwa wakalale baada ya saa tano, yamepitwa na wakati," Hapi amesema.

Amesema amemuagiza Katibu Tawala wa Mkoa wa Iringa, Happiness Seneda kuitisha kikao kitakachowashikilisha wafanyabiashara hao na Polisi ili kufikia muafaka wa mambo muhimu ya kuzingatia kabla uamuzi wake huo haujaanza kutekelezwa.

"Moja ya mambo yanayosikitisha Iringa, ikifika saa tatu usiku hukuti watu barabarani. Tunaposema mji wa kitalii, tunataka uchangamke hauwezi kuchangamka kama sehemu za burudani zitaendelea kudhibitiwa zifanye biashara kwa saa hizo chache," amesema