Serikali yapongezwa kwa kuanzisha kliniki tembezi


Wananchi wa Kijiji cha Kikombo katika Halmashauri ya Jiji la Dodoma wameishukuru Serikali ya Awamu ya Tano kwa kuanzisha huduma yakiliniki tembezi ambayo inatoa huduma za afya karibu na maeneo wanayoishi jamii.


Hayo yamesemwa na Diwani wa Kata ya Kikombo, Yona Kusaja wakati wa uzinduzi wa kiliniki tembezi uliyofanyika leo katika Kituo cha afya Kikombo kilichopo katika Kijiji cha Kikombo, Kata ya Kikombo, Halmashauri ya Jiji la Dodoma.

Kusaja amesema kuwa ujio wa kiliniki tembezi umesaidia kwa kiasi kikubwa kuwepo kwa wataalam waliobobea katika magonjwa mbalimbali hivyo kuwafanya wananchi wengi kujitokeza kwa ajili ya kufanyiwa vipimona kupatiwa tiba kwa haraka na wakati kwa gharama nafuu.

“Wazee wengi wamejitokeza kuja kuchunguzwa afya zao jambo ambalo linatia moyo, kutokana na huduma hizo kusogezwa karibu na wananchi na wanatumia gharama ndogo kutibiwa” Amesisitiza Kusaja.

Akizindua Kiliniki hiyo Tembezi Mkuu wa Wilaya ya Dodoma, Patrobas Katambi amewaomba wananchi kutokuwakatisha tamaa watoa huduma za afya nchini bali wawatie moyo kwa kuwa wanafanyakazi ngumu ya kuokoa jamii hivyo hawana budi kuwaombea na kuwajali watumishi hao.

“Watumishi wa kada ya Afya wanafanyakazi katika mazingira magumu ya kuwahudumia wagonjwa na kuficha siri zao, hivyo ifike wakati wananchi watambue kuwa kazi hiyo ni ya kujitolea hivyo tuwatie moyo na kuwaombea kwa mwenyezi mungu” Amesisitiza Katambi.

Katambi amewataka watumishi wa afya kufanya kazi kwa weledi kwa kuzingatia maadili ya utumishi wa umma wa kuwajali na kuwahudumia wananchi kwa upendo ili waweze kuvutiwa na huduma zinazotolewa katika vituo vya kutolea huduma za afya nchini.

Amesema kuwa ni wajibu wa watoa huduma za afya nchini kuhakikisha wanatoa huduma bora za afya na zenye viwango kwa jamii ili kupunguza malalamiko katika Sekta ya Afya nchini.

Wakati huohuo Afisa Ustawi wa Jamii Bi. Shekilaga Nkinda kutoka Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (ambaye pia ni Mlezi wa Timu za Afya Mkoa wa Dodoma) amewaomba wananchi kuhakikisha wanakitumia kituo cha afya cha Kikombo kwa kuwa ni mali yao na kimejengwa kwa ajili ya kuwapatia huduma bora za afya.