Songwe kuanza kuzalisha chumvi itakayouzwa ndani na nje ya nchi



Na, Baraka Messa, Songwe.

 Kiwanda cha Chumvi cha Itumbula kata ya Ivuna wilayani Momba Mkoani Songwe kuanza kuzalisha chumvi mwishoni mwa mwezi huu ambayo itasambazwa ndani na nje ya nchi ambazo ni wanachama wa Jumuiya ya Maendeleo nchi zilizo kusini mwa Afrika (SADC) ili kuongeza mapato ya halmashauri hiyo , mkoa na Taifa kwa ujumla

akiongea kwenye Ziara ya kamati ya Siasa ya Mkoa wa Songwe chama cha Mapinduzi(CCM) Mkuu wa mkoa wa Songwe Brigedia Jeneral Mtaafu Nicodemas Mwangela alisema kiwanda hicho kitaanza kuzalisha rasmi Chumvi mwishoni mwa mwezi huu.

alisema mradi huo wa uzalishaji chumvi unategemewa kuwa mkubwa ambao utazalisha chumvi ambayo itatumika ndani ya mkoa wa Songwe, ndani ya taifa na katika nchi jirani hasa za kusini mwa Afrika .

"mradi huu wa chumvi kuna uwezekano ukawa mkubwa kuliko hata ule wa uvinza, soko la uhakika kwa upande wa chumvi lipo ndani ya nchi yetu na nyingine tuziuzia nchi za kusini mwa Afrika zilizopo kwenye Jumuiya ya SADC " alisema Mwangela.

"tarehe 22 mwezi huu chumvi itakuwa tayari na nitakuja kuchukua baadhi uya packet za kwanza kwa ajili ya matumizi yangu na viongozi hawa wa kamati ya Siasa mkoa " aliongeza

Mwenyekiti wa kamati ya Siasa chama cha Mapinduzi mkoa wa Songwe Elniko Mkolla alisema ahadi za Chama cha mapinduzi ilikuwa ni pamoja na kutengeneza ajira kwa vijana hivyo anategemea kuwa vijana wengi watapata ajira kupitia mradi huo wa Chumvi.

pia aliiagiza serikali ya mkoa wa Songwe kutatua baadhi ya changamoto zilizopo katika kiwanda hicho ikiwepo changamoto ya miundo mbinu ya barabara ili mradi uweze kuanza haraka na kunufaisha wakazi wa Momba na nchi kwa ujumla.

Kwa upande wake Mkurugenzi  mtendaji wa Halmashauri ya Momba Adrian Jungu alisema kuwa mradi huo mpaka kukamilika utagharimu jumla ya shilingi na milion 535 utakuwa na uwezo wa kuzalisha jumla ya tani 50 mpaka 60 kwa mwaka.

"mradi huu utakuwa na manufaa makubwa sana kwa halmashauri yangu kwa sababu mapato yataongezeka lakini pia vijana zaidi ya 4,000 watapata ajira katika kiwanda hiki cha chumvi " alisema Jungu.

Osca Benson ni mkazi wa kijiji cha Itumbula alisema tayari mradi huo umeanza kuwapatia ajira za mbali mbali ambazo zinawapelea kupata kipato ambacho kinawasaidia katika familia zao.

aliitaka Serikali ya Mkoa ikishirikiana na viongozi wa wilaya kukamilisha haraka mradi huo ili uweze kuwanufaisha zaidi kwa kupata kazi nyingi ikiwa ni za ujenzi kutengeneza vitalu na kazi nyingine za kiwandani pindi kitakapo anza kufanya kazi.