Tamko la Serikali kuhusu kupiga mnada Viboko, Mbunge Gekul afunguka


Na John Walter, Babati

Baada ya tamko la serikali la kupiga Mnada Viboko, Watembeza watalii wa nadani na nje ya nchi katika ziwa Babati  wameomba  iwapunguze na sio kuwapiga mnada wote.

Wavuvi na wanaofanya shughuli zao ziwa Babati wanaseama hatua hiyo itawasidia kufanya kazi zao kwa amani na uhuru zaidi kwani mara nyingi wamekuwa wakivua kwa hofu kwa sababu ya kuhofia viboko hao.

Hata hivyo hatua hiyo  itakuwa tofauti kwa wanaowatembeza watalii katika ziwa hilo kuwatazama Viboko.

Watembeza watalii hao ambao hutumia Mitumbwi yao ya makasia wamesema viboko hao wamekuwa ni chanzo cha wao kuingiza kipato ambacho kinasiadia kuendesha familia zao.

Wakati wakiyazungumza hayo,wananchi wanaoishi pembezoni mwa ziwa hilo wamekuwa na kilio cha muda mrefu wakitaka viboko hao waondolewe kwa kuwa wamewaua  ndugu na jamaa zao huku wengine wakiachwa yatima na wajane.

Maeneo yalioathiriwa sana na Viboko hao ni Nakwa,Bagara ziwani,Himiti,Nangara ziwani.

Hivi Karibuni Waziri wa Maliasili na Utalii, Dk Khamis Kigwangala amesema Serikali itaanza kuuza asilimia 10 ya mamba nje ya nchi kutokana na ongezeko kubwa la wanyama wakali kuingia kwenye makazi ya watu.

Vilevile Serikali itauza viboko wote waliopo kwenye maeneo yenye maji kama maziwa, mabwawa na mito iliyopo mjini.

Waziri amesema Serikali imejitahidi vya kutosha kuhakikisha suala la ujangiri linaisha nchini na wamefanikiwa kwa kiasi kikubwa bali changamoto iliyopo, ni wanyama hao kuingia kwenye makazi ya watu.

Hata hivyo Mbunge wa  Jimbo la Babati mjini (CCM) Paulina Gekul ameipongeza serikali kwa hatua hiyo huku akitaka hatua zichukuliwe mapema.

Amesema katika vikao vyake maeneo ya Ziwa Babati,kilio kikubwa cha wananchi  ni fidia kwa walioathiriwa na wanyama hao hivyo serikali kwa kufanya hivyo itaondoa malalamiko hayo.

Serikali itauza viboko wote waliopo kwenye maeneo yenye maji kama maziwa, mabwawa na mito iliyopo mjini, kama vile pale Mpanda, Mafia na Babati. Mauzo ya wanyama hawa yatafanyika kwa njia ya mnada.