Tanzania kufanya jitihada Kiswahili iwe lugha ya SADC


Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Profesa Palamagamba Kabudi amesema katika Mkutano wa 39 wa wakuu wa nchi na Serikali na kwenye mwaka mmoja ujao Tanzania itafanya jitihada kuhakikisha Kiswahili kinakuwa lugha rasmi ya nchi wanachama wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC).

Waziri Kabudi ameyasema hayo jijini Dar es Salaam baada ya kukabidhiwa uenyekiti wa Baraza la Mawaziri wa nchi za SADC na ataifanya kazi hiyo kwa mwaka mmoja.

Profesa Kabudi amewaeleza waandishi wa habari kuwa, katika mwaka mmoja ujao, SADC pia itaendeleza harakati za kuitaka jumuiya ya kimataifa ishinikize Zimbabwe iondolewe vikwazo vya kiuchumi.

"Zimbabwe imewekewa vikwazo vya kiuchumi kwa muda na tunadhani vikwazo hivyo havina sababu ya kuendelea kwa sababu Zimbabwe imekwishafanya uchaguzi, Rais amechaguliwa na maendeleo wananchi wanaendelea vizuri sasa ni wakati wa vikwazo vya kiuchumi kuondolewa kwa Zimbabwe ili Zimbabwe iendelee,"amesema Waziri Kabudi.

Profesa Kabudi anaongoza mawaziri SADC akichukua jukumu hilo kutoka kwa Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Mambo ya Nje Namibia Netumbo Nandi-Ndaitwah.

"Kwa nchi zetu kubadilisha uchumi wetu ni lazima tuendeleze sekta yetu ya viwanda ili kuongeza nafasi za ajira, na kupunguza umaskini na suala hili lazima lifanywe kwa utengamano," amesema Waziri Kabudi baada ya kukabidhiwa jukumu hilo.

Amesema, kwa sasa biashara baina ya nchi wanachama SADC ni chini ya asilimia 20, hivyo kuna kazi kubwa ya kubadili hali hiyo ili kuongeza biashara ndani ya SADC kwa kutengeneza mazingira wezeshi.