Tanzanite kupambana na Wakenya


Kocha wa timu ya Taifa ya Tanzania ya wanawake wenye umri chini ya umri wa miaka 20, Tanzanite, Bakari Shime amewapongeza wachezaji wake kwa kutwaa ubingwa wa mashindano ya COSAFA na kuwataka kuelekeza akili katika mchezo wa kirafi ki wa kimataifa dhidi ya Kenya unaotarajiwa kuchezwa Agosti 15, 2019 Nairobi.

Akizungumza kwa njia ya mtandao , Shime alisema lilikuwa lengo lake kutwaa ubingwa wa mashindano hayo na anamshukuru Mungu kwa kufanikiwa kutimiza azma hiyo.

“Nilijiandaa kwenda kushindana ili turudi na ubingwa na siyo kushiriki na namshukuru Mungu wachezaji wamefuata maelekezo na hatimaye tumekuwa mabingwa,” alisema Shime.

Pia alisema baada ya kurejea timu hiyo itaingia kambini moja kwa moja na leo wachezaji aliowaita kwenye kikosi cha Twiga Stars wataondoka kwenda nchini Kenya kucheza mchezo wa kirafiki na Harambee Starlets.

Amewataka wachezaji wote watakaokuwa nchini Kenya wajue wanaipeperusha bendera ya taifa hivyo ni wajibu wao kupigana kwa ajili ya taifa kwa kuweka uzalendo mbele. Tanzanite ilirudi jana ikitokea Port Elizabeth, Afrika Kusini ilipokuwa ikishiriki mashindano ya Cosafa.

Katika mashindano ya Cosafa, Tanzanite kwenye hatua ya makundi ilipata ushindi mechi mbili 2-0 dhidi ya Botswana, 8-0 dhidi ya eSwatini na kupoteza mchezo mmoja na Zambia kwa mabao 2-1.

Katika nusu fainali ilifunga Afrika Kusini kwa mabao 2-0 na fainali ikakutana tena na Zambia na kufanikiwa kulipa kisasi kwa kuifunga 2-1 kwenye Uwanja wa Wolfson.

Mbali na Kombe, Tanzanite walipata medali za dhahabu na nahodha wake Enekia Kasonga aliibuka kuwa mchezaji bora wa mashindano.

Katika kikosi kinachoondoka leo, Shime amewajumuisha wachezaji 13 kutoka kikosi cha Tanzanite, ambao ni makipa Tausi Abdallah, Janeth Shija, Enekia Kasonga, Fumukazi Nguruwe, Opa Clement, Irene Kisisa, Protasia Pius, Emeliana Mdimu, Diana Lucas, Ester Mabanza, Janeth Christopher, Vailet Thadeo na Phelomena David.

Wengine ambao walikuwepo Twiga ni kipa Najiat Abbas, Fatuma Issa, Happy Hezron, Donisia Minja, Stumai Abdallah, Asha Hamza, Amina Ally, Fatuma Mustapha, Mwanahamisi Omary na Aisha Masaka.