Ujenzi wa soko la kisasa Njombe wafikia 75%



Na Amiri kilagalila-Njombe

Halmashauri ya mji wa Njombe mkoani Njombe inaendelea kufanikisha ujenzi wa soko kuu na la kisasa ambapo mpaka sasa ujenzi umefikia asilimia 75 licha ya mkandarasi kukabiliwa na changamoto mbali mbali za ujenzi ikiwemo upatikanaji wa kokoto.

Akizungumza na waandishi wa habari mhandisi msimamizi wa ujenzi wa soko hilo Mboka justin lwambogo licha ya kukabiliwa na changamoto katika ujenzi huo wanatarajia kukamilisha ifikapo oktoba 28 mwaka huu endapo halmashauri itakamilisha haraka baadhi ya vitu muhimu vinavyohitajika katika soko hilo.


“Tumeongezewa mda wa ujenzi mpaka 28 mwezi wa 10,tunategemea tukamaliza kwa kuwa kwenye swala la ujenzi huwa kuna ujenzi,lakini pia kwenye jengo letu kuna upande ambao unatakiwa ujengwe ukuta wa kuzuia udongo usishuke chini,hivyo ni baadhi ya vitu ambavyo vipo ndani ya mda umeongezeka lakini kama vitatatuliwa kwa haraka zaidi tunaweza tukamaliza jengo kwa mda huo”alisemaMboka justin

Hata hivyo wakati ujenzi wa soko la kimataifa mkoani humo ukiwa ukingoni kumalizika katika mji wa Njombe,baadhi ya wafanyabiashara walioondoshwa kupisha ujenzi huo na kupelekwa katika soko la Dodoma akiwemo Victoria uhahula,Hawa mohamed na Oresta kigora wameendelea kulalama wakidai wamezika mitaji yao.

“Huku kwa kweli bado hali ni mbaya tunakaa toka asubuhi tunauza 1000 hamna biashara,sisi tunaomba serikali itukamilishie mapema soko lile turudi maana mitaji yetu kama mnavyoona tumezika”alisema Oresta kigola mmoja wa wafanyabiashara.

Edwirn mwanzinga ni mwenyekiti wa halmashauri ya mji wa Njombe amesema endapo soko hilo litakamilika baada ya kumuongezea muda mkandarasi wa kampuni ya Nandra kutokana na sababu mbalimbali litakwenda kuwa mkombozi katika uchumi wa wananchi mjini humo.

“Badala ya kumaliza lile soko mwezi wa nane tumejikuta sasa mkandarasi inabidi aende mpaka mwezi wa kumi,kama atakwenda vizuri na ninaimani anakwenda vizuri kwasababu shughuli zilizo nyingi zinakamilika na wafanyabiashara wa Njombe watuvumilie kwasababu lile soko likiisha kutakuwa na mabadiliko makubwa sana kuanzia muonekano wa mji”alisema Mwanzinga.

Hadi kukamilika kwa ujenzi wa soko hilo litatumia zaidi ya shilingi bilioni 9 huku likiwa na meza za chini 404 maduka 161 pamoja na eneo la mgahawa wa vip na mgahawa wa mama lishe soko ambalo litachukua zaidi ya wafanyabiashara 1000.