Ujerumani yakataa kuungana na Marekani

Waziri wa Mambo ya Kigeni wa Ujerumani Heiko Maas amesema hii leo kwamba Ujerumani haitaungana na ujumbe wa kijeshi unaoongozwa na Marekani katika lango la bahari la Hormuz lakini akisema Berlin inauunga mkono kuundwa kwa ujumbe wa Umoja wa Ulaya ingawa ameonya kuwa ni vigumu kupiga hatua.

Maas amewaambia waandishi wa habari kwamba, Uingereza inaweza kuungana na Marekani kwa sasa, lakini Ujerumani haitafanya hivyo na kusema wanataka kuungana na ujumbe wa Ulaya.

Ubalozi wa Marekani mjini Berlin ulisema Jumanne iliyopita kwamba umeiomba Ujerumani kuungana na Ufaransa na Uingereza katika operesheni za kulinda safari za meli kupitia Hormuz na kukabiliana na uchokozi wa Iran.

Waziri wa Mambo ya Kigeni wa Iran Mohammad Javad Zarif amesema Marekani sasa inabakia peke yake wakati washirika wake wakiona aibu kuungana na vikosi vyake kwenye eneo la Ghuba huku akipuuzilia mbali mwito wa mazungumzo na Washington.