Waandamanaji waivamia ofisi ya tume Algeria

Waandamanaji nchini Algeria hii leo wameyavamia makao makuu ya tume iliyopewa jukumu la kushughulikia mdahalo wa kitaifa na kuandaa uchaguzi wa urais unaonuiwa kumaliza miezi kadhaa ya mgogoro wa kisiasa.

Mwezi Aprili rais wa Algeria Abdelaziz Bouteflika alijiuzulu kufuatia wiki kadhaa za maandamano dhidi ya uongozi wake wa miongo miwili na shinikizo kutoka kwa jeshi lililo na nguvu nchini humo.

 Tangu wakati huo maandamano yamekuwa yakiendelea, kutaka maafisa wa utawala wa Bouteflika-kuwajibishwa akiwemo rais wa mpito Abdelkader Bensalah.

Mwezi uliyopita Bensalah aliunda tume hiyo ya mdahalo wa kitaifa inayoongozwa na aliyekuwa spika wa bunge Karim Younes.

Tume ilikuwa inakutana hii leo kuunda wataalamu watakaoshughulikia mdahalo huo. Waandamanaji walioandamana hii leo kuipinga tume hiyo pamoja na mkuu wake.

Wanaishutumu tume kwenda kinyume na matakwa ya watu wa Algeria na kupuuzia maandamano ya amani ya kitaifa yaliyoanza Februari 22.