Watumishi wa Umma waongoza kwa kudaiwa na Nyumba za TBA,zoezi la kuwaondoa laanza



Na,Enock Magali,Dodoma

Wakala wa Majengo nchini Tanzania (TBA),imeendesha zoezi la kuwaondoa wapangaji wote wasiolipa kodi katika majengo waliopangishwa ndani ya Mkoa wa Dodoma

Wapangaji hao ni Taasisi za umma na wafanyakazi wa Serikali ambao hadi hivi sasa TBA inawadai zaidi ya Shilingi Bilion 1.5.

Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dodoma mara baada ya kuendesha oparesheni ya kuwaondoa baadhi ya wapangaji wa maeneo ya Area C na D,Kaimu meneja wakala wa Majengo Mkoa wa Dodoma,Herman Tanguye amesema kuwa uendeshaji wa zoezi hilo umefata taratibu zote za kisheria ikiwa ni pamoja na kutoa notisi ya siku thelathini kwa wapangaji.


"Zozi hili tumelianza leo,baada ya kufuata taratibu zote za kisheria na mikataba inavyosema kwani tuliewapa notisi ya siku thelathini baada ya hapo tukawaongeza siku kumi na nne nazo zimkwisha kwaiyo tumechukua vyombo ambavyo vinatambuliwa na mahakama ili tuweze kuwaondoa"Alisema.


Kwa upande wake Kaimu meneja wa Miliki Fredy Mangula amesema zoezi hilo wameanzia Mkoani Dar es Salaam na wanatarajia kulifanya kwa nchi nzima lengo likiwa ni kukusanya madeni yote ili waweze kufanya maendelezo mengine katika nyumba hizo kwani pia uhitaji wa Nyumba umeongezeka mara baada ya Serikali na watumishi wa Taasisi mbalimbali kuhamia Mkoani Dodoma.

"Zoezi hilo limeanzia Dar es Salaam lakini kwa sasa limehamia hapa Mkoani Dodoma kwa sababu ndipo kuna deni kubwa lakini pia itafanyika nchi nzima  kwaiyo nitoe rai kwa wale wote wenye madeni na waliopewa notisi waweze kulipa hayo malimbikizo kwa muda waliopewa kwani kumekuwa na mazoea ya wapangaji kupewa notisi lakini kumekuwa hakuna utekelezaji"Alisema.

Aidha katika kukabiliana na ongezeko la uhitaji wa nyumba za watumishi katika Mkoa wa Dodoma Mangula amesema kuwa TBA wamejipanga kuhakikisha kuwa wanakabiliana na changamoto hiyo na mapema iwezekanavyo wanatarajia kuanza ujenzi katika eneo la Nzuguni jijini Dodoma.