Na,Enock Magali Dodoma
Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) Selemani Jafo amemuagiza Katibu Mkuu Tamisemi Mhandisi Joseph Nyamhanga kuwarudisha watumishi saba waliohamishwa kutoka kwenye kituo cha afya cha Ipogoro kilichopo Manispaa ya Iringa na kupelekwa kituo kingine kwa madai ya usimamizi mbovu wa fedha.
Aidha amemuagiza pia kufuatilia suala la Mganga Mkuu wa wilaya ya Bumbuli Mkoani Tanga aliyesimamishwa kazi ili kujua kama kusimamishwa kwake ni kushindwa kufanya kazi au ni majungu.
Akifungua kikao kazi cha waganga wakuu wa mikoa na halmashauri leo jijini Dodoma Jafo amesema madaktari wanafanya kazi usiku na mchana tusipowalinda tutakuwa hatuwatendei haki.
Amesema mganga mkuu yoyote akifanya vibaya ahukumiwe kwa makosa yake lakini yule anayetengenezewa majungu basi alindwe.
Kwa upande wake Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Dokta Faustine Ndugulile amehimiza suala la kuimarisha utoaji wa huduma bora za afya.
Mkurugenzi wa Idara ya Afya,Ustawi wa Jamii, lishe kutoka Tamisemi dokta Ntuli Kapologwe ameeleza lengo la kikao hicho huku Mwenyekiti wa waganga wakuu wa mikoa dokta Paul Chawote ameiomba serikali kuendelea kuboresha miundombinu ya vituo vya afya.
Kauli mbiu ya kikao hicho cha siku 5 inasema Uwajibikaji ni nguzo muhimu katika utoaji wa huduma bora za afya kuelekea uchumi wa kati.