Waziri Mkuu wa Uingereza akataa wazo la kuitisha bunge la dharura

Waziri Mkuu wa Uingereza Boris Johnson amekataa wazo la kuitisha kikao cha bunge cha dharura kujadili suala la nchi hiyo kujiondoa Umoja wa Ulaya, Brexit, katika wakati huu wabunge wakiwa kwenye mapumziko ya majira ya kiangazi.

Kiongozi wa chama kikuu cha upinzani cha Labour, Jeremy Corby, alitoa wito huo baada ya kuvuja kwa ripoti ya serikali inayotahadharisha juu ya kutokea uhaba wa chakula na dawa nchini Uingereza ikiwa nchi hiyo itajiondoa Umoja wa Ulaya bila ya mkataba tarehe 31 mwezi Oktoba.

Ripoti hiyo iliyochapishwa kwenye gazeti la Sunday Times inatahadharisha juu ya kutokea vurumai kubwa katika ugavi wa dawa, uhaba wa chakula, na maji safi.

Hapo awali waziri kivuli wa fedha, John McDonell, alisema kuwa Corbyn atakutana na wanasiasa wengine wiki ijayo kujadili suala hilo.

Wakati huo huo, Waziri Mkuu Boris Johnson anatarajiwa kukutana na Kansela Angela Merkel wa Ujerumani na Rais Emmanuel Macron wa Ufaransa ili kuujadili upya mkataba wa Brexit.