Dkt. Mafumiko: Gharama ya uchunguzi wa vinasaba (DNA) ni Sh. Laki Moja kwa kila mmoja

Mkemia Mkuu wa Serikali Dkt. Fidelis Mafumiko amesema kuwa uchunguzi wa vinasaba (DNA) katika maabara ya mamlaka hiyo hufanyika ndani ya siku 21 pekee na sio zaidi ya hapo huku gharama ya uchunguzi huo wa vinasaba ikiwa ni shilingi laki moja kwa kila sampuli.

Ameyasema hayo Dkt.Mafumiko wakati akifunga mafunzo maalumu ya siku mbili kwa waandishi wa habari jijini Dar esSalaam yaliyolenga kuwajengea uwezo waandishi wa habari juu ya majukumu ya mamlaka ya Maabara ya Mkemia mkuu wa Serikali (GCLA).

“Ni siku 21 pekee ndizo zinazotumika kuchunguza vinasaba mbalimbali na sio zaidi ya hapo labda itokee janga la dharura kama lile la moto Morogoro ambalo ilitulazimu kutumia siku kumi usiku na mchana kwa kufuata hatua zote ili kupata vinasaba na kuweza kuwapumzisha wapendwa wetu.” Ameeleza Dkt. Mafumiko.

Dkt.Mafumiko amesema kuwa mamlaka hiyo ina dawati la malalamiko ambalo lipo wazi wakati wote kuwahudumia wananchi na amesisitiza kuwa huduma zote za kiuchunguzi wa kimaabara kutoka katika mamlaka hiyo zinatoka kwa vibali maalumu kwa kuzingatia sheria na kanuni.


Mkurugenzi wa idara ya sayansi, jinai na vinasaba (DNA), Khadija Mwema amesema kuwa uchunguzi huo hufanywa na makundi mbalimbali kwa kuwahusisha madaktari wenye sifa na waliosajiliwa na kutambulika na Serikali, wakemia wenye sifa na askari wa jeshi la polisi kuanzia ngazi ya Inspekta na hufanywa kwa kuzingatia kanuni, sheria na taratibu.

Mwema ameeleza kuwa majukumu ya mamlaka hiyo yamegawanyika katika maeneo makuu matatu ambayo ni uchunguzi wa kimaabara wa sampuli na vielelezo mbalimbali, utekelezaji wa sheria tatu ambazo mamlaka hiyo inazisimamia pamoja na kutoa ushahidi wa kitalaamu kwenye masuala yanayohusu uchunguzi wa kimaabara katika mahakama mbalimbali nchini.

Mamlaka hiyo ambayo ni maabara ya rufaa ilyoanza mwaka 1895 na kuwekeza zaidi katika mitambo, wataalamu na kuimarisha maabara katika kanda zote sita imekuwa ikitekeleza majukumu yake kwa kuzingatia afya, haki, amani na utulivu kote nchini.

Mwandishi mwandamizi kutoka Michuzi Blog, Chalila Kibuda kwa niaba ya waandishi ameiomba mamlaka hiyo kuendelea kutoa mafunzo maalumu kwa waandishi wa habari ili kuwajengea uwezo zaidi wa kuandika kwa mapana na kwa weledi kuhusiana na mamlaka hiyo kwa manufaa ya jamii na taifa kwa ujumla.

Mamlaka hiyo imekutana na wahariri na waandishi wa habari kutoka vyombo mbalimbali zaidi ya 100 ambao wamepata nafasi ya kufahamu kwa kina zaidi kuhusiana na majukumu yanayotekelezwa na mamlaka hiyo.