IGP Sirro afanya mabadiliko kwa Ma-RPC


Mkuu wa Jeshi Polisi nchini Tanzania (IGP), Simon Sirro amefanya mabadiliko madogo ya
makamanda wa polisi wa mikoa (RPC).

Msemaji wa Jeshi la Polisi nchini, David Misime amesema katika mabadiliko hayo Wilbroad Mutafungwa amehamishiwa makao makuu akitoka Morogoro. Misime amesema nafasi ya Mutafungwa imechukuliwa na Hamisi Issa aliyekuwa Kilimanjaro.

Ameongeza kuwa Saidi Hamdani aliyekuwa Njombe amehamishiwa Kilimanjaro na Mkuu wa Upelelezi Mkoa wa Geita, Daniel Sillah anakwenda kuwa Kamanda wa Polisi Njombe.

“Mabadiliko haya ni ya kawaida katika kuboresha utendaji kazi wa jeshi la polisi,” amesema Misime Ingawa pia amesema mabadiliko hayo ni ya kawaida lakini huenda kwa Kamanda wa Polisi wa Morogoro yamefanyika ikiwa ni utekelezaji wa maagizo ya Waziri Mkuu wa Tanzania, Kassim Majaliwa aliyoyatoa Bungeni jijini Dodoma.

Ikumbukwe Septemba 13, 2019 wakati akiahirisha mkutano wa 16 wa Bunge la 11 hadi Novemba 3,2019 Bungeni jijini Dodoma, Majaliwa alisema kamati aliyoiunda kuchunguza ajali ya lori la mafuta ya petroli iliyotokea Agosti 10, 2019 mkoani Morogoro imekamilisha shughuli yake.