Jonas Mkude ampigia debe Etienne Ndayiragije

Kiungo wa Taifa Stars, Jonas Mkude, amesema kuwa, kaimu kocha mkuu wa kikosi hicho, Etienne Ndayiragije, hivi sasa anafaa kabisa kukabidhiwa rasmi kikosi hicho baada ya kufanya vizuri.

Ndayiragije anakaimu nafasi hiyo baada ya kuondoka kwa Emmanuel Amunike ambapo tayari kocha huyo ameiongoza Taifa Stars katika mechi nne na kufanya vizuri.

Wikiendi iliyopita, Ndayiragije aliiongoza Taifa Stars kutinga hatua ya makundi ya kufuzu Kombe la Dunia baada ya kuiondosha Burundi kwa penalti 3-0.

Championi Jumatano, Mkude alisema kocha huyo amekuwa anaishi vizuri na wachezaji ndiyo maana wanapata matokeo mazuri.

“Kwa muda ambao tumekaa na Ndayiragije tumebaini kwamba ni kocha mzuri na mwenye kujali wachezaji wake, hana shida na mtu.

“Lakini pia ufundishaji wake ni mzuri, utaona katika mechi tulizocheza hadi sasa chini yake hakuna hata moja

tuliyoboronga. Hivyo anafaa kuwa kocha wetu rasmi,” alisema Mkude ambaye pia ni kiungo wa Simba.