Kituo cha msaada wa kisheria chanusuru Nyumba ya kikongwe


Na Ahmad Mmow, Lindi

Juhudi za wasaidizi wa msaada wa kisheria kwa wanawake na watoto cha NYAPAU zimesababisha kunusuru nyumba ya Tecla Nangungulu (85) isiuzwe bila hiari yake.


 Akizungumza na Muungwana Blog katika kijiji cha Nyangao, halmashauri ya wilaya Lindi. Tecla ambae alianza kwa kushukuru NYAPAU alisema nyumba yake ilikuwa katika hatari ya kuuzwa na mjukuu wake baada ya mjukuu wake huyo kuanza kupangisha. Wakati yeye akiwa kwenye matibabu.

Alisema mjukuu wake huyo anayetambulika kwa jina la David alipangisha hata chumba cha kikongwe huyo.  Hali iliyosababisha akose mahali pakulala.

Tecla huku akiwa na huzuni alisema David alimwambia nyumba hiyo haimuhusu na fedha zilizokuwa zinalipwa nawapangaji zilikuwa haki na halali yake.

"Nilikosa mahali pakulala, nilipomuuliza alikuwa anasema nyumba hiyo hainihusu. David niliyemlea tangu akiwa mtoto mchanga nakuishinae kama mwanangu alinigeuka na kutaka kunidhulumu nyumba niliyojenga kwa nguvu na jasho langu,'' alisema kwa masikitiko Tecla.

 Alipoulizwa aliwezaje kurudi na kuishi kwenye nyumba hiyo, alisema wasaidizi wa kituo cha msaada wa kisheria walimsaidia na kufanikiwa kukabidhiwa nyumba yake. Nibaada ya yeye kwenda kuomba msaada katika kituo hicho kinachotoa msaada wa kisheria katika wilaya ya Lindi yenye kata 31.

Mratibu wa kituo hicho Fransis Chijinga alisema nyumba hiyo ilikuwa katika hatari ya kuuzwa na David. Hata hivyo walimuita na kumpa elimu kwakumuonya kwamba kitendo hicho nikosa kwa mujibu wa sheria na niwajibu wake kumtunza kikongwe huyo badala ya kumdhulumu na kumnyanyapaa.

Chijinga alisema elimu hiyo ilimtosha kijana huyo ( 31) ambae alikiri kwamba nyumba hiyo aliyokuwa anaipigia hesabu za kuuza ni mali ya bibi yake huyo.

Kwa upande wake, David alisema ujana na tamaa vilisababisha amtendee ukatili bibi yake ambae alimlea baada ya mama yake huyo.

"Nashukuru kwa elimu niliyopewa, niliharibika. Polisi na rumande kulikuwa kama nyumbani, lakini hawa wamekuwa walimu wazuri, nimetulia hadi nafanyabiashara ya  kuuza nyama ya nguruwe,'' alisema David.

Kijana huyo alisema hivi sasa anamtunza kikongwe huyo. Huku akiweka wazi kwamba njia pekee ya kujikwamua na umasikini nikufanyakazi kwa juhudi na maarifa.

Nae ofisa mtendaji wa kata ya Nyangao, Mahfoudh Salum Ali alisema uwepo wa wasaidizi wa kisheria umeipunguzia mzigo ofisi yake kupokea na kushughulikia migogoro. Hasa inayohusu matunzo ya watoto, ndoa, mirathi na talaka.

 ''Wametutua mzigo, kwani migogoro mingi inasuluhiswa na wasaidizi wa kisheria. Huko hata ikipelekwa migogoro mia moja, basi tisini na nane inapata suluhisho,'' alisema Mahfoudh.


Kituo hicho  nimiongoni mwa vituo vilivyo katika halmashauri zote zilizopo katika mkoa wa Lindi. Vituo ambavyo shughuli zake zinaratibiwa na kusimamiwa na shirika la msaada wa kisheria kwa wanawake na watoto wa Lindi( LIWOPAC).