https://monetag.com/?ref_id=TTIb Kituo cha msaada wa kisheria chasaidia kupunguza mimba na utoro shuleni | Muungwana BLOG

Kituo cha msaada wa kisheria chasaidia kupunguza mimba na utoro shuleni



Na Ahmad Mmow-Lindi

Elimu inayotolewa na wasaidizi wa kituo cha huduma za msaada wa kisheria cha NYAPAO katika shule ya msingi Nyangao imesaidia kupunguza tatizo la utoro na mimba kwa wanafunzi wanaosoma katika shule hiyo.

Hayo yameelezwa na mwalimu mkuu msaidizi wa shule hiyo, Faraja Chilemba. akizungumza na Muungwana Blog, jana  katika kijiji cha Nyangao, mwalimu Chilemba alisema kituo hicho kimesaidia kupunguza tatizo la mimba kwa wasichana na utoro katika shule hiyo.

 ''Wanatembelea sana shuleni nakuzungumza na wanafunzi, wasichana wanafundishwa masuala ya mimba za utotoni na hedhi salama. Elimu wanayopewa inawafanya waipende shule na kuepuka vitendo vinavyosababisha mimba, wanatusaidia na kutupunguzia kazi,'' alisema Chilemba.

Mmoja wa wasaidizi wa kisheria wa NYAPAO, Martina Chikoko alisema ushirikiano wanaopewa na viongozi, wataalamu na watendaji wa serikali za vijiji, kata na wilaya unawafanya wajione wanadeni kubwa kwa wananchi.

''Tulibaini kwamba baadhi ya wasichana wanapokuwa kwenye siku zao hawaendi shuleni, kwa hiyo tunawafundisha hedhi salama na wajitambue,'' alisema Chikoko.

Ofisa mtendaji wa kata ya Nyangao, Mahfoudh Salum Ali alisema kituo hicho ni msaada mkubwa kwa ofisi yake katika kusuluhisha na kutatua migogoro ya wananchi katika kata hiyo.

 '' Lakini hawa wanahudumia kata 31 za wilaya ya Lindi, hawana hata usafiri, wanashindwa kuwafikia kwa wakati wananchi waliombali na hapa Nyangao. Kwa hiyo sisi kama serikali tumepokea, pale uwezo utakaporuhusu kusaidia na kutatua changamoto hiyo,'' alisema.