Masheha watakiwa kujua majukumu yao



Na Thabit Madai,Zanzibar

Masheha wa Wilaya Kusini Unguja wametakiwa kujua majukumu ambayo yanayowapasa kukabiliana nayo pindipo yakitokea maafa katika shehia zao ili kupunguza adhari zinazoweza kujitokeza.

Hayo yameelezwa  na  Mkuu wa Kitengo cha Mipango na Rasilimali Watu kutoka Kamisheni ya Kukabiliana na Maafa, Haji Faki Hamdani wakati wa kikao cha  kutathmini hali ya majanga katika shehia za Wilaya ya Kusini Unguja na Wenyeviti  wa kamati ya kukabiliana na maafa.


 Alieleza kuwa  Masheha wa shehia mbao ndio wenyeviti wa kamati ya kukabiliana na maafa  iko haja ya  kuongoza zoezi la kuondoa au kupunguza viashiria vya majanga katika shehia husika pamoja na kutoa elimu ya kukabiliana na maafa katika shehia zao.

 Alifahamisha kuwa masheha waweze  kuielimisha  jamii njia sahihi za mawasiliano wakati wa dharura inapotokea  pia kutenga eneo la makazi wakati wa dharura ndani ya Shehia zao .

Aidha alisema janga ni tukio ambalo linaweza kupelekea maafa na kusababisha adhari kubwa kwa jamii na vilevile maafa ni tukio kubwa ambalo linapelekea adhari ikiwemo vifo na upotevu wa mali.

Mkuu huyo aliwataka masheha kuwa pamoja na jamii hasa kwa wale ambao wamepatwa na majanga ili kuweza kuwafariji pamoja na kushajihisha wengine kwa kuweze kuwasaidia .

“Rasilimali watu ni hazina kubwa kwa maendeleo ya shehia na nchi kiujumla hivyo jamii iweze kuweka tahadhari katika majanga ambayo yanasababishwa na binaadamu “.alisema  Mkuu huyo .

Hata hivyo alisema kuna majanga ambayo huwezi kuyaepuka ambayo yanasababishwa na majanga ya kimaumbile ikiwemo kimbunga ,mvua kubwa za mafuriko mtetemeko wa ardhi na mengineyo hayo husababisha vifo na upotevu wa mali kutokana na mabadiliko ya tabia ya nchi .

Nae Mkuu wa Kitengo cha Elimu Ushauri Nasaha na Tafiti Haji Ame Haji amewataka wenyeviti hao kuratibu ufanyaji wa tathmini ya awali juu ya athari iliyojitokeza baada ya maafa na ripoti iwasilishwe kwa wahusika pamoja na kufahamisha  aina ya mahitaji wanayohitajia wahanga .

Vilevile mkuu wa kitengo cha elimu huyo  aliwataka wenyeviti hao kutunza kumbukumbu za matukio ya majanga yanayotokea katika shehia zao  ili kusaidia kurejesha hali kulingana na uwezo wao.

Kwa upande wa wenyeviti hao wamesema kuwa wanakazi kubwa kuielewesha jamii kwani wananchi hawajui  majanga wala ajali  wanachotaka wao wafanye wapendalo .

Wenyeviti hao waliiyomba Serikali za Halmashauri kufika katika maeneo ya shehia zao ili kuona hali halisi ya mpango miji inayojengwa na kuweza kutoa ushauri kwa wananchi .

 Wenyeviti hao walisema  kuwa Sheha ni jina kubwa lakini halina kitu hivyo wakati mwengine hupata wakati mgumu kwa jamii ambapo  huwa ni tegemeo lao kubwa la  kupata kupewa mkono wa pole .