Mbinu za kuongeza au kuvutia wateja kwenye Biashara

Haijalishi huduma au bidhaa yako ni kubwa kiasi gani, biashara yako haitazalisha pesa kama wateja hawatakuwa tayari kununua bidhaa au huduma yako. Hakuna wateja, hakuna biashara.

Tatizo la kukosa wateja hukabili sana biashara ndogo, na hata kusababisha biashara hizo kufa. Siyo kwamba wateja hawapendi kununua bidhaa za biashara hizi, bali tatizo kubwa ni mbinu duni za kujitangaza na masoko.

Katika makala hii nitakueleza mbinu  rahisi na za gharama nafuu ambazo unaweza kuzitekeleza na ukaongeza au kuvutia wateja zaidi kwenye biashara yako.

Lugha nzuri
Katika mambo yanayowapotezea wafanyabiashara wengi wateja ni lugha mbaya kwa wateja. Hakuna mteja anayependa kupokelewa au kujibiwa vibaya.

Hakikisha unazungumza na wateja wako kwa namna bora ambayo wataona unawajali, unawathamini na kuwaheshimu.

Mimi mwenyewe ninapenda kwenda kwenye biashara ambayo wahusika wana lugha nzuri; huwa nawashauri pia rafiki zangu kwenda kwenye biashara za aina hiyo. Hivyo hakikisha unatumia mbinu hii ili kuongeza wateja.

Huduma au bidhaa za bure
Wateja wengi wanapenda vitu vya bure au zawadi. Siyo lazima ufanye jambo kubwa la bure ili kuwavutia wateja; hata jambo dogo tu linaweza kuwavutia sana.

Ili kuwavutia wateja unaweza kutoa huduma au vitu vya bure kama vile kalamu, mifuko, shajara (diary) au hata maji ya kunywa. Kwa njia hii utawavutia wateja wengi zaidi.

Punguzo
Punguzo ni njia bora sana ya kukabiliana na ushindani wa kibiashara na kupata wateja. Ikiwa mwenzako anauza sabuni kwa shilingi 2,100, wewe uza 2,050. Unaweza usipate faida kubwa kwenye bidhaa moja lakini utapata faida kubwa kwenye mauzo ya jumla.

Kwa mfano ikiwa faida kwenye sabuni hapo juu ni sh. 100, muuzaji wa kwanza akauza sabuni 5 kwa sh. 2,100 atapata faida ya sh. 500.

Lakini wewe ukauza sabuni 20 kwa sh. 2,050 utapata faida ya sh. 1,000. Je huoni kuwa umeuza na kupata faida zaidi kutokana na kuvutia wateja wengi kupitia punguzo? Weka punguzo sasa.

Tumia mitandao ya kijamii
Kama ilivyo kwa blog na tovuti, vivyo hivyo mitandao ya kijamii inaweza kutumiwa kuzalisha pesa nyingi.

Ikiwa unataka kuongeza wateja, basi wafahamishe watu kupitia mitandao ya kijamii juu ya huduma au bidhaa zako. Hakikisha wanazielewa na kuweza kuzifikia kwa urahisi.

Matangazo
“Biashara ni matangazo.”

Biashara nyingi hupuuza nafasi ya kujitangaza ili kuongeza wateja na hatimae kupata faida zaidi. Siyo lazima utumie njia za gharama kubwa kujitangaza kwani zipo njia nyingi sana.

Unaweza kutumia mitandao (rejea mbinu ya 5 na 6), vifungashio, saini ya barua pepe (email signature), card ya utambulisho wa biashara (busness card), vipeperushi n.k.

Lenga changamoto
Watu wananunua bidhaa au huduma fulani ili itatue changamoto zao. Hivyo kuendesha biashara isiyolenga changamoto za wateja haitapata soko.

Hivyo ili kuongeza wateja hakikisha unakuwa mbunifu na kulenga changamoto na mahitaji ya wateja.