Polisi yawatawanya waandamanaji wanaompinga Rais Al Sisi

Mamia ya waandamanaji walijitokeza mjini Cairo na miji mingine ya Misri jana usiku wakitaka Rais Abdel Fatah Alsisi aondoke madarakani.

Picha za video za maandamano hayo, zinazowaonesha mamia ya waandamanaji wakisema "Ondoka Sisi", zilisambazwa mtandaoni zikiwa na hashtag #Tahrir_Square.

Hata hivyo, polisi walijitokeza na kuwatawanya waandamanaji hao. Kwa mujibu wa mwandishi wa shirika la habari la AFP alishuhudia takribani waandamanaji watano wakiwekwa chini ya ulinzi, huku polisi wakiwarushia waandamanaji mabomu ya machozi katika uwanja wa Tahrir.

Maandamano kama hayo ni nadra kutokea nchini humo tangu serikali ilipopitisha sheria inayopiga marufuku maandamano. Sheria hiyo ilipitishwa baada ya jeshi la Misri kumwondoa madarakani aliyekuwa Rais wa nchi hiyo, aliyechaguliwa kwa njia za kidemokrasia Mohammed Morsi.

Maandamano hayo yamefanyika baada ya mfanyabiashara wa nchi hiyo aishiye uhamishoni kutaka Al Sisi aondoke madarakani kwa tuhuma za rushwa.

Hata hivyo Rais Alsisi alikanusha madai hayo wiki iliyopita na kusema yeye ni mkweli na mwaminifu.