https://monetag.com/?ref_id=TTIb Serikali yaanza maandalizi ya kushusha bei ya umeme | Muungwana BLOG

Serikali yaanza maandalizi ya kushusha bei ya umeme


Waziri wa Nishati na Madini, Dk Medard Kalemani amesema serikali inatarajia kufanya mabadiliko ya gharama za bei ya umeme na gesi asilia viwandani.

Hivyo ametoa mwezi mmoja kuangaliwa upya gharama za bei ya gesi asilia viwandani huku mabadiliko ya gharama za umeme yakitarajia kufanyika baada ya kukamilika kwa mradi mkubwa wa uzalishaji umeme kwa maji kwani gharama za uzalishaji zitapungua.

Kalemani alisema hayo wakati akizindua matumizi ya gesi asilia katika kiwanda cha Lodhia Plastic Industries Limited kinachozalisha mabomba ya plastiki na nondo kilichopo Mkuranga Mkoa wa Pwani kinachotumia futi za ujazo za gesi asilia 200,000 kwa siku.

Waziri alibainisha kuwa mpaka sasa viwanda 48 vinatumia gesi asilia ambayo inapunguza gharama za uzalishaji kwa asilimia 50 hadi 30 ukilinganisha na matumizi ya mafuta mazito.

Alisema baada ya kukamilika kwa miradi mikubwa ya umeme yatafanyika mapitio ya gharama ya kununua umeme jambo litakalofanya bila shaka kushuka kwa bei ya umeme hivyo kutaka uongozi wa kiwanda wanaotaka ruzuku ya asilimia tano kwa kununua megawati 14 za umeme kusubiri mabadiliko hayo.

Alisema uwekezaji gesi asilia viwandani hauchangamki inawezekana kuna vikwazo mbalimbali lakini bei ya kununua gesi inaweza kuwa changamoto kwani kwa sasa ni dola 4.7 hadi 7.72 kwa uniti

Alitoa mwezi mmoja kwa Shirika na Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC), Mamlaka ya Udhibiti wa Nishati na Maji (EWURA), Mamlaka ya Udhibiti wa Mkondo wa Juu wa Petroli (PURA), wataalam wa wizara na wanasheria husika kufanya mapitio ya bei ya gesi viwandani kama ni kikwazo kwa wawekezaji kutumia gesi asilia.