Wanaomiliki meno ya Tembo kinyume na sheria watakiwa kujisalimisha


Serikali imetoa muda wa mwezi mmoja (kuanzia Septemba 4 hadi Oktoba 4, 2019) kwa wananchi wote wanaomiliki meno ya Tembo kinyume cha sheria, kuhakikisha wanayasalimisha kwenye vyombo vya ulinzi na usalama na kwamba watakaofanya hivyo kabla ya kuisha kwa muda huo hawatashtakiwa.

Waziri wa Maliasili na Utalii, Dkt. Hamisi Kigwangalla ametoa muda huo alipokuwa akizungumza na waandishi wa Habari jijini Dar es salaam mara baada Kikosi Kazi cha Taifa dhidi ya Ujangili (NTAP) kukamata watuhumiwa 8 wa ujangili, vipande 338 na meno mazima ya Tembo 75 pamoja  na meno mawili ya kiboko.

“Nimewaita hapa ili mshuhudie kazi nzuri iliyofaywa na maafisa wa Serikali na Kikosi Kazi maalum cha kudhibiti ujagili, ninatoa huruma ya mwezi mmoja kwa kila aliye na meno ya Tembo ayasalimishe kwenye chombo chochote cha Serikali na atakayefanya hivyo ndani ya muda huo hatutamshtaki” Amesisitiza Dkt.Kigwangalla.

Dkt. Kigwangalla amesema kukamatwa kwa majangili hao kumetokana na kazi ya muda mrefu ambayo imezaa matunda na matokeo yake kuonekana kwa kukamatwa kwa majangili sugu 8 (nane) akiwemo Bw. Hassan shaban maarufu kwa jina la Nyoni aliyekuwa akitafutwa kwa muda mrefu kwa kujihusisha na mtandao wa ukusanyaji wa meno ya Tembo kutoka Tanzania na Msumbiji.

Amesema  mtuhumiwa huyo wa ujangili amekamatwa na jumla ya vipande vya meno ya Tembo 338 na memo mazima 75 pamoja pamoja na meno 2 ya Viboko ambapo kwa mujibu wa Wataalam na Wanasayansi wa Uhifadhi wa Wanyamapori wanaeleza kuwa meno hayo ni sawa na Tembo 117 waliouawa.

Amebainisha kuwa meno hayo yalianza kutafutiwa soko mwaka 2015 wakati Serikali ya Awamu ya Tano ya Rais Dkt. John Pombe Magufuli ilipoingia madarakani, hivyo hatua ya Serikali kuimarisha  Ulinzi wa Rasilimali za Taifa  na kukiongezea uwezo Kikosi cha Kudhibiti Ujangili soko la meno hayo liliharibika.

Dkt. Kigwangalla amesema katika kipindi cha Serikali ya Awamu ya tano Majangili wengi wamekamatwa na mitandao yao kusambaratishwa akisisitiza kuwa yeyote atakayejihusisha na biashara hiyo kwa namna yoyote ile atakamatwa na kufikishwa kwenye vyombo vya Sheria.

“Mtuhumiwa huyu amehangaika na huu mzigo kwa zaidi ya miaka minne na hili nataka watanzania wajue ya kwamba yeyote atakayejihusisha na biashara hii ya kuuza nyara za Serikali tutamkamata tu maana, sababu ni moja wateja tumebaki ni sisi wenyewe popote utakapojaribu kuuza tutakukamata tu”

Aidha, ametoa onyo kwa wananchi wanaojihusisha au kushiriki kwa namna yoyote ile  na vitendo vya ujangili waache mara moja akibainisha kuwa kazi hiyo kwa sasa haina nafasi nchini Tanzania.