Waziri Lugola awataka Askari kuacha mara moja tabia hii


Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Kangi Lugola amewataka baadhi askari na wananchi kuacha tabia ya kuwatuhumu viongozi wanapowatetea waendesha bodaboda wanaambiwa kuwa wanasiasa ndiyo wanasababisha ajali kuongezeka.

Waziri Lugola ameyasema hayo Mjini Moshi, leo, wakati alipokuwa anakagua vituo vya bodaboda na bajaj mjini humo ambapo mwezi uliopita alifanya mkutano na wamiliki na waendesha bodaboda na bajaj mkoani humo.

Amesema kauli hiyo sio sahihi, kwani wanaosababisha ajali asilimia 76 kwa mujibu wa utafiti wa ajali zinazotokea barabarani zinasababishwa na makosa ya wanadamu na sio bajaj na bodaboda peke yao, na asilimia 24 za ajali zinatokea zinasababishwa na ubovu wa miundombinu.

“Kumekuwa na dhana potofu kwamba wanasiasa kama mimi tunasababisha ajali za bodaboda, kwasababu tunawatumia bodaboda kwa mgongo wa siasa, sasa nataka niwaambie, wanaosababisha ajali barabarani ni asilimia 76 ni makosa ya wanadamu ambao ni wanadamu watembea kwa miguu, waendesha baiskeli, wenye mikokoteni, wanafuga mifugo barabarani na madereva ndio wanasababisha ajali, na sio bodaboda wala bajaj peke yao,” alisema Lugola.

Lugola amesema hakuna mahali popote ambayo tumesema baodaboda wakifanya makosa wasikamatwe, tunachosema na kusimamia nikupunguza umaskini kwa mujibu wa Ilani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), ambapo inaelekeza Bodaboda na Bajaj wafanye biashara ili wapunguze umaskini.
 
Aidha, Lugola amesema Serikali ya Magufuli inataka wananchi Watanzania wajiajiri hivyo sekta ya bodaboda lazima iheshimika kwakua nao wanatafuta ridhiki kama ilivyo kwa watanzania wengine.