Boris akwama kuitoa Uingereza Umoja wa Ulaya Oktoba 31


Mchakato wa Uingereza kujitoa kutoka Umoja wa Ulaya ifikapo Oktoba 31, mwaka huu umeonekana kukwama baada ya bunge la nchi hiyo kumtaka Waziri Mkuu, Boris Johnson kutuma barua ya maombi kwa Umoja wa Ulaya (EU) kuchelewesha kuondoka kwa nchi yake katika umoja katika tarehe hiyo.

Nakala ya barua hiyo haikuwa na saini yake, hivyo ombi hilo limeambatanishwa na barua ya pili, iliyotiwa saini na Waziri mkuu huyo, akisema anaamini ucheleweshaji wa kujitoa ni kosa.

Ndoto ya Uingereza kujitoa kutoka Umoja wa Ulaya kwa tarehe iliyokuwa imepangwa inaonekana kutoweka. Hii ni baada ya Waziri Mkuu kutakiwa na sheria kuiomba EU kuongeza muda zaidi baada ya kushindwa katika kura ya bunge ambalo limepinga mpango mbadala uliokuwa umeandaliwa na Johnson wa kujitoa ifikapo Oktoba 31, mwaka huu.

Rais wa Baraza la EU, Donald Tusk ameandika kupitia ujumbe wa tweeter kwamba amepokea barua ya maombi ya kuongezewa muda na amesema atashauriana na viongozi wa EU namna gani ya kujibu ombi la Uingereza.

Wabunge wa upinzani wamemuonya waziri mkuu kwamba iwapo atajaribu kukwepa maelekezo ya Bunge kutaka kuchelewesha tarehe ya kuondoka EU, basi atajikuta akifikishwa mahakamani.

Awali Johnson alinukuliwa akisema ni bora afe kuliko kuiomba EU icheleweshe mpango wa Brexit, huku akijiapiza kuwa kwa vyovyote itakavyokuwa Uingereza lazima iondoke EU ifikapo Oktoba 31 hata bila ya mkataba unaoeleweka.

Saa kadhaa baada ya kupoteza kura katika kikao cha kihistoria kufanyika Jumamosi, waziri mkuu alimwagiza mwanadiplomasia mwandamizi kutuma nakala ya barua isiyotiwa saini kwenda EU kuomba kuongezewa muda.

Barua hiyo ni ile ambayo wabunge walimtaka waziri mkuu aitume EU lakini hakufanya hivyo akiamini kuwa mpango wake mbadala utaiwezesha Uingereza kuondoka EU ifikapo tarehe hiyo.

Mkwamo huu ni ule ambao pia uliwahi kumpata mtangulizi wake Theresa May ambaye alishindwa kutimiza masharti ambayo yangeiwezesha Uingereza kujitoa EU huku kila upande ukinufaika.

Masuala kadhaa yameonekana kikwazo kwa Uingereza kuondoka EU bila ya mikataba inayoeleweka likiwemo la mpaka wa Ireland ya Kaskazini.