DC awataka viongozi wa dini kuendelea kumuombea Rais Magufuli


Mkuu wa Wilaya ya Ikungi, Edward Mpogolo amewataka viongozi dini kuendelea kumuombea Rais Dkt.John Magufuli kutokana na kazi kubwa anayoifanya ya kutekeleza miradi ya maendeleo.

Mpokolo alitoa ombi hilo hivi karibuni alipokuwa mgeni rasmi kwenye mkutano wa hadhara wa kuliombea Taifa na uchaguzi wa serikali za mitaa ulioandaliwa na Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania ( KKKT) Usharika wa Mang’onyi Dayosisi ya Kati mkoani Singida.

”Viongozi wa dini mnafanya kazi kubwa ya kuifanya nchi yetu kuwa na amani na utulivu kutokana na kuiombea  na viongozi wake endeleeni kufanya hivyo na kumuombea Rais wetu kwani anafanya kazi kubwa ya kutuletea maendeleo katika nchi” alisema Mpogolo.

Mpogolo alisema Rais Magufuli ametekeleza miradi ya maji, umeme, ujenzi wa reli, vituo vya afya na zahanati zaidi ya 350, ununuzi wa ndege 11 katika sekta ya elimu ujenzi wa madarasa na kutoa elimu bure kuanzia darasa la kwanza hadi sekondari.

Aliongeza kuwa katika wilaya hiyo ametoa sh. 720 milioni kwa ajili ya kujenga kituo cha afya cha kisasa Kata ya Ihanja,  Kata ya Sepuka  sh.400 milioni, Kata ya Iyumbu sh. 500 milioni  na hospitali ya wilaya sh. Bilioni 1.500, 000,000 na kuwa  serikali imeanza kutandaza umeme wa Wakala wa Nishati ya Umeme Vijiji (REA) awamu ya tatu katika wilaya hiyo baada ya kusambaza nguzo.

Alisema kutokana na kazi hiyo kubwa anayoifanya Rais Magufuli anatakiwa  kuombewa ili awe na afya njema na kuendelea kuchapa kazi ya kuwatumikia wananchi.