DC Msafiri aagiza mwenyekiti wa serikali ya mtaa kuhojiwa



Na Amiri kilagalila-Njombe

Mkuu wa wilaya  ya Njombe Bi.Ruth Msafiri amemwagiza mrakibu wa jeshi la polisi wilaya ya kipolisi Makambako Limited Mhongole kumtafuta na kumhoji mwenyekiti wa serikali ya mtaa wa sokoni mjini Makambako Alfan Kawambwa  kwa tuhuma za kuvuruga zoezi la uandikishaji wa daftari la wapiga kura kwa kumsumbua mwandishi wa zoezi hilo.

Akizungumza katika ofisi ya mtaa wa sokoni Msafiri amesema,mwenyekiti anatakiwa kukamatwa na kuhojiwa kwa kuwa amefika kwenye kituo hicho na kumsumbua msimamizi wa zoezi bila utaratibu na kueleza kuwa ikiwa kamanda wa polisi hatalidhishwa na maelezo ya mwenyekiti huyo anaruhusiwa kumweka ndani na kumfungulia mashtaka kwenye vyombo vya kisheria ili akawajibishwe.

“Mwenyekiti ambaye yupo katika kumalizia muda wake alidiriki kufika katika kituo hiki na kutaka kupekua na kuangalia nyaraka za serikali kinyume na utaratibu,kwa maana hiyo kwa kweli amekuja hapa kuvuruga zoezi zima la uchaguzi,nimeagiza OCD Makambako ambaye ndiye mwenye eneo hili aweze kuchukua hatua juu ya huyu, amtafute na kumhoji kama hata ridhika na maelezo yake nimetoa kibali cha kumuweka ndani na kumfungulia mashtaka kwa mujibu wa taratibu aende akajibu kwa nini aliingia kuja kuvuruga zoezi hili ambalo linaendeshwa kwa mujibu wa utaratibu na sheria zilizowekwa”alisema Msafiri

Awali akizungumza na mkuu wa wilaya msimamizi wa zoezi hilo la uandikishaji kwenye daftari la mpiga kura katika kituo hicho cha sokoni Morad Myinga amesema amekutana na changamoto kutoka kwa mwenyekiti wa mtaa huo ambaye anatokana na chama cha demokrasia na maendeleo( CHADEMA ) ambaye amefika katika kituo hicho na kumtuhumu kuwa mwandikishaji huyo ni mwanachama wa chama cha mapinduzi na kupekua daftari kuona watu ambao wamejiandikisha.

Askari mgambo anayesimamia kituo hicho Aujensi Mlengule amesema mwenyekiti wa mtaa huo wa sokoni alifika ofisini hapo na kumwambia atoke nje ili awapishe kwa madai ya kwamba anamazungumzo na mwandikishaji huyo.

“Aliniomba niwapishe azungumze na muandikishaji basi niliwapisha nikasimama eneo la tukio mbele ya mlango, baada ya hapo kulikuwa na majibizano kati ya yeye na mwandikishaji wa wapiga kura na baadaye akatoka,kwa mujibu wa kiapo changu kisheria hakutenda haki”Alisema Mlengule