Faida za mmea wa mzambarau kiafya

Katika nchi yetu ya Tanzania, tunazo  aina nyingi sana za miti katika maeneo tunayoishi au hata katika mashamba yetu, ya ndugu na jirani zetu.

Wengi wetu inatusaidia kwa kutupa kivuli na matunda tu, hatujui kuwa ni msaada mkubwa mno kwa afya zetu.

Miongoni mwa miti hiyo ni mti wa mzambarau. Mzambarau si mti maarufu sana lakini unapatikana katika maeneo mengi. Mizambarau ipo ile ya kupandwa na mingine huota yenyewe mwituni mara nyingi katika maeneo yenye asili ya majimaji.

Mti huu unasaidia sana kwa wale wenye maradhi ya vidonda vya tumbo, wanaosumbuliwa na kisukari, unasaidia kuondoa maumivu ya miguu inayowaka moto, wenye uoni hafifu kuweza kuona vizuri, wanaotapika na kuharisha nao wanaweza kupona baada ya kutumia mti huo.

Licha ya kuwa mti huu ni tiba kwa ujumla kwa maana ya majani, magome, matunda na mizizi, maradhi tajwa yote yanatibiwa kwa magome.

Namna ya kutumia; chukua vipande vya magome ya mzambarau vichemshe kwa muda wa dakika 15 kunywa maji yake kikombe kimoja cha chai mara mbili kutwa (asubuhi na jioni).

Au unaweza kukausha gombe kisha kusaga unga wake ambao unaweza kuutumia katika uji mwepesi au maji moto kikombe kimoja cha chai asubuhi na jioni.