Maandalizi ya Mkutano wa Mawaziri SADC yakamilika


Na Ferdinand Shayo-Arusha

Maandalizi ya Mkutano wa Mawaziri wa Mazingira, Maliasili na Utalii wa nchi mwanachama wa SADC unaotarajiwa kuanza kesho jijini Arusha  yamekamilika na tayari wageni kutoka mataifa mbalimbali wameanza kuwasili.

Mwenyekiti wa Kamati ya Maandalizi ambaye ni Katibu Mkuu wa Wizara, Profesa Adolfu Mkenda amesema kuwa maandalizi tayari yamekamilika kuanzia eneo ambalo mkutano huo utafanyikia katika ukumbi wa kimataifa wa mikutano wa AICC, usafiri, chakula pamoja na fursa ya kutembelea Hifadhi mbalimbali za Taifa.

Profesa Mkenda amesema kuwa siku ya kesho makatibu wakuu wa Wizara husika watakutana na kuandaa agenda za mkutano huo ambao mpaka sasa maandalizi yamekamilika.

Naibu Katibu Mkuu, Wizara ya Kilimo, Maliasili, Mifugo na Uvuvi Zanzibar  Dr. Omar Ali Amir ameeleza kuridhishwa na maandalizi yaliyofanyika mpaka sasa na Tanzania kama mwanachama wa SADC imeweka mikakati ya kushirikiana katika kupambana na uvuvi haramu baharini.