Mamlaka ya Hali ya Hewa watoa utabiri wa Mvua


Mamlaka ya Hali ya Hewa nchini(TMA), imetoa utabiri wa muelekeo wa mvua za msimu Novemba hadi Aprili 2019/2020 na kusema kuwa mvua zinazotarajia kunyesha katika maeneo mengi yanayopata msimu mmoja wa mvua kwa mwaka zinatarajia kuwa za wastani hadi juu ya wastani.

Huku mvua nyingi inatarajia kunyesha katika nusu ya kwanza ya msimu kutokana na uwezekano wa uwepo wa upepo kuvuma kutoka upande wa magharibi.

Akizungumza Dar as Salaam akitoa utabiri wa msimu huo, Mkurugenzi wa TMA, Dkt. Agness Kijazi alisema upepo huo unatarajia kubeba unyevunyevu Kutokana misitu ya Kongo kuelekea katika maeneo ya nchi yetu.

Alisema kwa upande wa kipindi cha nusu ya pili cha msimu mvua zinatarajiwa kupungua katika baadhi ya maeneo kutokana na joto la bahari sehemu ya kati ya bahari ya Hindi kuendelea kuongezeka ikilinganishwa na maeneo mengine ya bahari ya Hindi.

“Mvua za msimu ni mahsusi katika maeneo ya magharibu mwa nchi ,kanda ya kati ,nyanda za juu kusini magharibi,kusini mwa nchi,ukanda wa pwani ya kusini pamoja na maeneo ya kusini mwa mkoa wa Morogoro ambapo maeneo haya yanapata msimu mmoja wa mvua ambazo zinaanza mwezi Novemba hadi Aprili ya mwaka unaofuata,” alisema Dkt.Kijazi

Alisema katika mkoa wa Tabora mvua inatarajia kunyesha juu ya wastani hadi wastani huku mkoa wa Kigoma na Katavi inatarajia kunyesha mvua za wastani hadi juu ya wastani na kutarajia kuanza wiki ya nne ya mwezi Oktoba 2019katika mkoa wa kigoma na kusambaa Kwa mikoa ya Katavi na Tabora katika wiki ya kwanza ya mwezi Novemba.

“Mvua katika maeneo ya Singida na Dodoma zinatarajia kuanza katika wiki ya Kwanza hadi wiki ya pili ya mwezi Novemba 2019 na maeneo mengi yanatarajiwa kupata mvua za juu ya wastani hadi wastani,” alisema na kuongeza

“Katika mikoa ya Rukwa, Songwe, Mbeya, Iringa, Njombe, Ruvuma pamoja na maeneo ya kusini mwa mkoa wa Morogoro mvua zinatarajia kuanza kati ya wiki ya kwanza na ya pili ya mwezi Novemba 2019 na kutarajia kuwa za juu ya wastani hadi wastani katika maeneo mengi,” alisema

Aidha alisema katika mikoa ya Lindi na Mtwara mvua zinatarajia kunyesha kati ya wiki ya kwanza na wiki ya pili ya mwezi Novemba 2019 na zinatarajia kuwa za juu ya wastani hadi wastani.

Dkt. Kijazi alisema kuwa matukio ya vipindi vifupi vya mvua kubwa yanaweza kujitokeza hata katika maeneo yanayotarajiwa kupata mvua za wastani.

Alisema migandamizo midogo ya hewa pamoja na vimbunga katika eneo la kusini magharibi mwa bahari ya Hindi inatarajiwa kuvuta upepo wenye unyevunyevu kutoka misitu ya Kongo na hivyo kusababisha mvua katika maeneo mengi hapa nchini.

Dkt. Kijazi ametoa ushauri Kwa watumiaji wote wa taarifa za hali ya hewa ikiwa ni pamoja na wakulima,wafugaji,mamlaka za wanyamapori,sekta za maji na afya kuendelea kufuatilia na kutumia ushauri wa kitaalam katika shughuli zao za kila siku.