Maofisa watendaji Kata na vijiji Ruangwa wapewa ushauri huu


Na Ahmad Mmow, Lindi

Maofisa watendaji kata na vijiji wilayani Ruangwa, mkoa wa Lindi wameshauriwa wasikimbilie kupeleka polisi na mahakamani mashauri yanayohusu madai.

Ushauri huo ulitolewa jana mjini Ruangwa na Mkurugenzi wa Shirika la msaada wa kisheria kwa wanawake na watoto wa Ruangwa( RUPAO), Menrad Lilai  alipozungumza na Muungwana Blog.

Lilai alisema ili kuzipunguzia mzigo wa kupokea na kusikiliza  mashauri mengi yanayosababisha  mrundikano wa mashauri kwenye idara hizo, watendaji hao wajenge utamaduni wakusuluhisha badala ya kuharakisha kupeleka katika idara hizo.

Mkurugenzi huyo alisema usuluhishi unatengeneza mahusiano mema katika jamii kuliko polisi na mahamani ambako baada ya kutolewa hukumu na adhabu kunakuwa na chuki.

''Jitihada za kusuluhisha ziwe kubwa, bali Inaposhindikana ndipo wapeleke mahakamani,'' alisema Lilai.

Alibainisha kwamba idara hizo zinapelekewa mashauri mengi. Kwahiyo kunahaja ya kuzipunguzia mzigo kwa kutatua migogoro kabla ya kupelekwa huko. '' Itakuwa vema wakajikita kupeleka mashauri ya kijinai na mauaji kwenye idara hizo ambazo zinaelemewa na wingi wa mashauri.

Kwabahati mzuri  halmashauri zote katika mkoa huu zina vituo vinavyotoa huduma ya msaada wa kisheria bila malipo, basi wapeleke kwenye vituo hivyo ikatatuliwe kwa njia ambazo zitadumisha mahusiano mema na mshikamano kwa jamii,'' alisisitiza Lilai.

Kuhusu hali ya migogoro katika wilaya ya Ruangwa, mkurugenzi huyo alikiri kwamba kuna migogoro mingi.  Hata hivyo wananchi wengi wanakimbilia katika ofisi za kata na vijiji kuliko kwenye vituo vya msaada wa kisheria.

Aliitaja migogoro inayoongoza kuripotiwa katika kituo hicho kuwa ni ardhi, mirathi na matunzo ya watoto.