RC Mahenge atinga Kanisani kuhamasisha uandikishaji


Wakati muda wa uandikishaji wa daftari la orodha ya wapigakura kwa ajili ya uchaguzi wa serikali za mitaa ukiongezwa, Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Dk. Binilith Mahenge, ameingia kanisani kuhamasisha wananchi kujiandikisha.

Viongozi wenzake katika ngazi ya wilaya waliingia mitaani kwa ajili ya kuwahamasisha wananchi kujitokeza katika mchakato huo.

Mkuu huyo wa Mkoa alifanya hivyo kwenye Kanisa la Waadventista Wasabato (SDA) Dodoma Kati. Licha ya kuhamasisha watu kujiandikisha, pia aliwataka kujitokeza kwa wingi kushiriki katika uchaguzi wa serikali za mitaa uliopangwa kufanyika Novemba 24, mwaka huu.

Alisema mkoa wa Dodoma unakadiria kuwa na watu milioni 2.3 na wanaotarajiwa kujiandikisha ni milioni 1.2 kwa ajili ya uchaguzi huo.