Serikali ya Trump yakataa kutoa ushirikiano wa kumshitaki Rais

Ikulu ya Marekani imesema serikali ya Rais Donald Trump haitatoa ushirikiano katika kile inachokiita uchunguzi usio halali wa kumshitaki rais uliopendekezwa na chama cha Democratic.

Katika barua iliyotumwa jana kwa viongozi wa bunge hilo mawakili wa serikali ya Trump wameeleza wazi kwamba hawatoshiriki.

Hatua ya kukataa kushiriki katika uchunguzi huo inaonesha kuwa Trump sasa anaweza kuingia katika mvutano wa kikatiba na bunge.

White House imesisitiza kwamba bunge halikupiga kura rasmi ya kuanza uchunguzi huo, na kuongeza kuwa kutokana na hilo linakosa mamlaka kamili ya kufanya mchakato wa kumshitaki Trump.

Akijibu barua hiyo spika wa bunge Nancy Pelosi amesisitiza kwamba bunge lina haki ya kikatiba ya kuzifuatilia taasisi za juu bila ya kuzingatia kura rasmi ya mchakato huo.