Serikali yajidhatiti kusimamia ustawi na maendeleo ya wazee nchini


Na Thabit Madai,Zanzibar

Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imesema itaendelea kusimamia Sera na Mipango yake madhubuti iliyojiwekea  yenye lengo la kuimarisha ustawi na Maendeleo ya wazee Nchini.

Kauli hiyo imetolewa leo  na Waziri wa Kazi, Uwezeshaji,Wazee,Wanawake na Watoto Zanzibar, Moudline Castiko kwa niaba ya Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk Ali Mohamed Shein katika kilele cha  Maadhimsho ya Siku ya wazee Duniani.

Maadhimisho hayo yalifanyika katika Ukumbi wa Hotel ya Zanzibar beach Resort iliyopo  Mazizini Mjini Magharib Unguja, huku  kauli mbiu kwa mwaka huu inasema ‘Tuimarishe usawa kuelekea Maisha ya Uzeeni’.

Waziri Castiko alisema Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imeanda Sera, mipango na mikakati mbali mbali  kwa  lengo la kuendeleza Ustawi na maendeleo ya wazee nchini ili wazee hao waishi maisha yenye furaha kutokana na mchango wao mkubwa katika kulitumikia taifa hili.

Alisema Sera na Mipango hiyo ni kama vile Dira ya Maendeleo ya mwaka 2020 (vision 2020) pamoja na Mkakati wa kukuza Uchumi na kupunguza Umasikini Zanzibar (Mkuza).

Waziri Castiko alieleza kuwa ili kutekeleza kwa  vitendo Mipango hiyo yote, Serikali imeandaa sera ya hifadhi ya jamii ambayo imeweka mikakati madhubuti ya kusimamia maendeleo ya Wazee nchini.

“Nyote ni mashahidi wa namna ambavyo Serikali iliyopo Madarakani hivi sasa inavyoendeleza jitihada hizo za kuwawekea mazingira mazuri wazee na kuimarisha ustawi na maendeleo yao” alieleza Waziri Kastiko.

Aliongeza kueleza kuwa miongoni mwa mikakati ya kuwaendeleza wazee ambayo inaendelea kuimarishwa na Serikali ya mapinduzi ya Zanzibar SMZ ni kuendelea kuwatunza wazee wasiokuwa na jamaa wala rasilimali.

“Sisi kama Serikali tumekuwa tukiwatunza wazee hao katika makao maalum yaliyoanzishwa kutoa huduma hiyo ambayo ni Sebleni, Welezo na limbani Pemba” alieleza Waziri huyo.

Katika maelezo yake alifafanua kwamba  hadi sasa kuna jumla ya wazee 76 wanaotunzwa katika makao hayo ambapo welezo 32, Sebleni 32, na limbani Pemba  wazee 8 ambapo wazee hao wanapatiwa huduma zote muhimu ikiwemo chakula, malazi mavazi, matibabu na Posho.

Katika hatua nyingine Waziri Castiko alitoa wito kwa jamii kutokwepa majukumu yao ya kuwalea wazee wao na kuwapeleka kulelewakatika majumba ya kulelea wazee.

“Wazee wanahitaji mapenzi na huruma kutoka kwa watoto na wanajamii inayowaznguka, Vibabu vya dini vitakatifu vinaeleza umuhimu na Baraka ya kuwatunza wazee hivyo si busara kuwatekeleza wazee wetu” alisema Waziri.

Aidha alisema kuwa kuishi na wazee ndani ya nyumba kunaleta Baraka na faraja kwa familia husika.

Mapema akisoma risala kwa niaba ya Wazee, Mzee Hamis  haji  Mkasaba kutoka Jumuiya ya Wazee Zanzibar alisema anaishukuru Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ) kwa namna inavyowajali wazee kwa kuwapatia huduma mbali mbali za kijamii.

Alisema Serikali imekuwa mstari wa mbele katika kuwajali na kuwatatulia changamoto mbali mbali ambazo zinawakabili takribani kila siku.

“Tunashukuru Mungu Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar inavyotujali kwa kutupatia huduma mbali mbali ikiwemo pensheni ya kila mwezi kwa kila Mzee Zanzibar “ alisema Mzee Mkasaba.

Katika Maelezo ya risala hiyo kwa niba ya wazee wanaomba kupatiwa nafasi ya kushiriki katika ngazi za maamuzi pamoja kupatiwa mikopo mbali mbali ambayo itawaendeleza kimaisha.

Maadhimisho ya Siku ya wazee Duniani huazimishwa kila mwaka  Duniani kote Ifikapo Octoba 1 ambapo siku hii hutumika kufanya tathimni ya changamoto zinazowakabili wazee Dunini Kote.