Sheria ya uwekezaji kubadilishwa


Serikali imeandaa mabadiliko makubwa ya sheria ya uwekezaji ili kuvutia zaidi mitaji ya sekta binafsi na kuboresha mazingira ya biashara.

Hayo yamesemwa Dar es Salaam na Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia Uwekezaji, Angela Kairuki alipokuwa akifungua mkutano wa tatu wa kimataifa sekta ya mafuta na gesi.

Kairuki amefungua mkutano huo kwa niaba ya Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa.

Mkutano huo wa siku mbili unahudhuriwa na washiriki 600 kutoka nchi mbalimbali duniani.

Amesema wanaifanyia marekebisho makubwa Sheria ya Uwekezaji ya mwaka 1997, kwa kuandaa mpango kabambe, ambapo vikwazo katika wizara vinaondolewa pamoja.

Aliwataka washiriki wa mkutano huo, waje kuwekeza Tanzania kwa sababu serikali imerahisisha sera za uwekezaji, imerekebisha sheria na hali ya kisiasa na kiuchumi inavutia kuwekeza. Alisema marekebisho ya sheria na sera mpya ya uwekezaji, yatawasilishwa bungeni katika Mkutano wa Novemba na aliomba wawekezaji hao kujiandaa kunufaika nayo kwa kuja kuwekeza.

Aliwataka wawekezaji kufanya kazi na serikali, kuwashirikisha wazawa uchumi wa mafuta na gesi kwa kuingia nao ubia, na kusaidia wanawake kushiriki, kwani wakipewa nafasi wanaweza pia. Aliwapongeza waandaaji wa mkutano, Ocean Business Partners, CWC Group na Wizara ya Nishati kwa kuuandaa kwa mafanikio kujadili changamoto, uzoefu na fursa za mafuta duniani.

Awali akimkaribisha Kairuki, Waziri wa Nishati, Dk Medard Kalemani alisema gesi ni muhimu kwa maendeleo ya nchi kwa sababu inatumika kupikia, magari, kufua umeme na katika miradi mikubwa inayotumia gesi asilia. Alisema wanaendelea na utafiti wa gesi Ruvu, Mnazibay, Songosongo na Bahari ya Hindi, ambako kuna tani za ujazo trilioni mbili na wameshatumia kiasi kidogo hadi sasa.