Waajiri watakiwa kuzingatia mpango wa mafunzo kwa Watumishi wa umma


Serikali imewataka waajiri nchini kuweka kipaumbele katika programu za mafunzo kwa Watumishi wa Umma ili kuwajengea uwezo kiutendaji kwa kuzingatia Kanuni za Maadili  ya kiutendaji.


Wito huo umetolewa na Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Dkt. Mary Mwanjelwa wakati wa kikao kazi chake na watumishi wa umma wa Halmashauri ya Wilaya ya Meatu, mkoani Simiyu kilichofanyika katika ukumbi wa Ofisi ya Halmashauri ya Wilaya hiyo.

“Waajiri hakikisheni mnatoa mafunzo kwa watumishi wenu ili kuendana na kasi ya Sayansi na Teknolojia ikiwa ni pamoja na kuendana na kasi ya Serikali ya Awamu ya Tano inayoongozwa na Dkt. John Pombe Magufuli ” Dkt. Mwanjelwa amesisitiza.

Dkt. Mwanjelwa ametoa wito huo baada ya kubaini kuwepo kwa uelewa mdogo wa masuala ya kiutumishi kwa baadhi ya watumishi wa umma wilayani humo.

“Nimegundua bado kuna ombwe la uelewa mdogo wa miiko ya kazi miongoni mwa watumishi wa umma unaosababisha kufanya kazi kwa mazoea, hivyo mafunzo yatawasaidia kuboresha utendaji kazi wao.” Dkt. Mwanjelwa ameongeza.

Aidha, Dkt. Mwanjelwa  ameitaka Tume ya Utumishi wa Umma kuwa na utaratibu wa kujiridhisha kama Waajiri wanawapeleka watumishi kupata mafunzo katika Chuo cha Utumishi wa Umma Tanzania ili wawe na ufanisi kiutendaji.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Meatu, Bw. Fabian  Manoza amemshukuru Dkt. Mwanjelwa kwa kufanya ziara wilayani hapo na kuahidi kutekeleza maagizo yote aliyoyatoa.

Dkt. Mwanjelwa amehitimisha ziara yake ya kikazi mkoani Simiyu iliyolenga  kuhimiza uwajibikaji kwa watendaji na watumishi wa umma ikiwa ni pamoja na kusikiliza kero za watumishi hao na kuzitatua.