Watuhumiwa wanane wapandishwa kizimbani kwa wizi wa mawe ya dhahabu Tarime



Na Timothy Itembe Mara.

Watuhumiwa (8) leo wamepandishwa kizimbani kwa makosa mbalimbali ikiwemo Uhujumu uchumi,Utakatishaji fedha na wizi wa madini ya dhahabu mali ya Mgodi wa ACACIA uliopo Nyamongo wilayani Tarime mkoani Mara.

Anesius Kainunura wakili wa serikali mwanadamizi ambaye pia ni mkuu wa mashitaka wilaya Tarime aliwataja waliosomewa mashitaka kuwa ni pamoja na Zabron John Seth 43,James Maharareri Makune 37,Jonarhan Chuwa Genji 27,Amosi Raphael Wahere 28,Mseti Chacha Isack 32,Chacha Marwa Ryoba 27,Petro Kegora Mariba 32 na Samson Mathayo Leonard 17.

Mwanasheria huyo aliiambia mahakama ya Wilaya Tarime kuwa watuhumiwa hao  wote kwa pamoja walitenda makosa hayo kwa nyakati tofauti katikati ya tarehe 15  Septemba hadi septemba 25 mwaka huu.

Kainunura aliongeza kuwa watuhumiwa hao wanatuhumiwa na makosa mbalimbali ikiwemo kula njala ya uhalifu wa kupangwa (Uhujumu uchumi) katika mgodi wa ACACIA uliopo Nyamongo kosa lingine ni kuiba mawe yenye uzito wa kilogramu 15 yenye dhamani ya shilingi Milioni 234 huku kosa lingine  linalowakabili  watuhumiwa hao ni la utakatishaji fedha.

Kwa upande mwingine Wakili alisema kuwa watuhumiwa namba 3 hadi namba 8 wote kwa pamoja wanakabiliwa na kosa la Utakatishaji fedha yaani kujipatia fedha isiyo halali ndani ya mgodi wa ACACIA kosa ambalo walilitenda  kati ya tarehe 22 hadi 25 mwaka huu  ya kupatikana na mawe yenye uzito wa kilogramu 15 yenye dhamani ya shilingi milioni 234.

Hakimu mkazi wa Mahakama ya wilaya Tarime mkoani hapa,Mohamed Robert alisema kuwa kutokana na mahakama hiyo kutokuwa na uwezo wa washitakiwa  wa makosa kama hayo washitakiwa hawatakiwi kujibu chochota ambapo watuhumiwa wamerudishwa Mahabusu hadi kesi itakapo tajwa Tarehe 23,10,2019.